Yanga SC yashusha presha kwa Marumo

08May 2023
Saada Akida
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yanga SC yashusha presha kwa Marumo

KOCHA Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze, ameitoa kauli ya kibabe kwa kusema kuwa hawana wasiwasi tena juu ya wapinzani wao katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF), Marumo Gallants ya Afrika Kusini baada ya kupata muda wa kutosha kuwaangalia katika mchezo wao dhidi ya Mamelod

 

 

Yanga inajiandaa kucheza na Marumo keshokutwa Jumatano kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya kurudiana Mei 17, mwaka huu nchini Afrika Kusini.

Marumo kwa sasa wanapambana kubakia katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini kutokana na kuwa kwenye hatari wa kushuka daraja licha ya kufanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo juzi Jumamosi ilikubali kichapo cha mabao 2- 0 kutoka kwa Mamelod katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Thohoyandou.

Akizungumza na Nipashe jana Kaze alisema wamepata muda wa kutosha wa kuwasoma wapinzani wao hao kuelekea katika mchezo wao, hali inayowapa matumaini makubwa ya kuweza kufanikiwa kupata ushindi wa kwenda katika hatua ya fainali ya michuano hiyo.

Alisema wamewaona wapinzani wao na kuona ubora na udhaifu wao na wana nafasi kubwa ya kumaliza mchezo kwenye Uwanja wa Mkapa, kwa sababu wamepata muda kuwaangalia katika mchezo wao mkubwa wa ligi juzi.

"Tumepata muda wa kuangalia mechi yao na walipoteza, hii imetusaidia kupunguza presha, lakini tumeweza kuona mapungufu yao yapo katika nafasi zipi ambazo zinaweza kutusaidia kupata ushindi,” alisema Kaze.

Aliongeza: “Ukweli wapinzani siyo wabaya na hatupaswi kuwadharau kutokana na nafasi waliyopo kwenye ligi ya kwao, kwa sababu ligi haina mtoano kama hii michuano ya CAF.

“Kikubwa tunaenda kucheza nao tukiwa hatuna presha kwa sababu tunajua tunaenda kucheza na mpinzani wa aina gani na yupo katika wakati gani, lakini tunachoweza kukiangalia upande wetu ni kutafuta matokeo ya ushindi."

Kikosi cha Yanga kinaendelea na mazoezi yao kwenye kambi yao Kigamboni Dar es Salaam kujiandaa na mchezo huo.