Safari ya Ulaya kumkimbiza Ulimwengu Mazembe

24Feb 2016
Mahmoud Zubeiry
Dar
Nipashe
Safari ya Ulaya kumkimbiza Ulimwengu Mazembe

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Ulimwengu amesema kengele kuhitimisha safari yake kucheza soka la kulipwa Afrika imelia na sasa anafukuzia nyayo za Mbwana Samatta kucheza soka Ulaya.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Ulimwengu.

Nyota huyo anayekipiga na mabingwa wa soka Afrika, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), amesema hatasaini mkataba mpya na klabu hiyo ya Lubumbashi mara ule wa sasa utakapokwisha Aprili mwaka huu.

“Inatosha kucheza Afrika, naipenda Mazembe, lakini sitaongeza mkataba mpya mwishoni mwa msimu huu (Aprili),” alisema jana Ulimwengu jana wakati akizungumza na Nipashe.

Mshambuliaji mwenzake waliokua kikipiga pamoja na TP, Samatta ametimkia Ulaya na kujiunga na klabu ya Genk inayocheza Ligi Kuu Ubelgiji.

Uliwengu anasema baada ya kushinda mataji nane nyumbani na Afrika akiwa na timu hiyo nambo moja kwa ubora barani Afrika, sasa ameamua kuwekeza nguvu kwenda kucheza soka nchi ya bara.

Ulimwengu aliyejiunga na Mazembe miaka minne iliyopita, hadi sasa ametwaa matatu ya Ligi Kuu ya DRC, matatu ya Super Cup ya DRC, moja la Ligi ya Mabingwa Afrika na moja la Super Cup ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

“Kwa ujumla maisha yangu yamekuwa mazuri sana Mazembe, najisikia furaha sana kutwaa mataji makubwa kama Ligi ya Mabingwa na Super Cup na pia kucheza Klabu Bingwa ya Dunia. Nadhani inatosha na sasa lazima niangalie changamoto zingine,” alisema.

Ingawa hakuwa tayari kueleze mwelekeo wake baada ya kuondoka Mazembe, lakini kuna taarifa kwamba huenda akaenda Ujerumani au Ufaransa.

Ulimwengu ilkuwa aondoke Januari mwaka huu, lakini Rais wa Mazembe, Moise Katumbi Chapwe hakuwa tayari kumuuza baada ya Samatta kuuzwa Ubelgiji.

Huenda mchezaji huyo akaondoka akiwa huru baada ya mkataba wake kumalizika Aprili, ingawa wakati huo Mazembe kwenye mashindano, hivyo kulazimika kubaki kwa makubaliano maalumu hadi Agosti.