Hata hivyo, mshambuliaji wa Simba, Jean Baleke anaonekana ndiye mchezaji ambaye ana nafasi nzuri zaidi ya kuisaidia timu yake kuondoka na ushindi huku kwa upande wa Yanga, mikoba ikiachwa kwa Stephanie Aziz Ki.
Baleke na Aziz Ki kila mmoja amefunga mabao 6, lakini Mkongomani wa Simba akitumia dakika chache uwanjani ukilinganisha na nyota huyo wa Yanga.
Kuelekea mechi hiyo, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema mchezo huo utakuwa na ushindani mkubwa kutokana na namna alivyowasoma wapinzani wake ambao hivi karibuni walikuwa katika mashindano ya kimataifa ya African Footbal League.
Gamondi alisema anafahamu mechi hiyo haitakuwa nyepesi kwa kila upande kutokana na maandalizi ambayo wamefanya na ubora wa wachezaji waliokuwa nao.
Kocha huyo alisema watacheza na timu nzuri na yenye uzoefu wa michezo mikubwa, hivyo wamejiandaa kuonyesha mchezo mzuri na kwa lengo la kutafuta matokeo chanya.
Alisema wanawaheshimu Simba lakini anajua kila mmoja anahitaji kushinda ili kujiweka katika nafasi nzuri katika mbio za ubingwa wa msimu huu.
"Tunaenda kutafuta alama tatu, tumesahau matokeo ya mechi ya kwanza, ulikuwa mchezo wa mwanzo wa msimu, uwanja haukuwa mzuri kwa timu zote kushindwa kucheza soka la aina tunayocheza.
Lakini Jumapili (kesho) tunaenda kucheza kwenye uwanja mzuri, mchezo utakuwa mzuri sana kwa sababu utakuwa wa kimbinu na kiufundi, ni wazi kila mmoja anahitaji matokeo chanya,” alisema Gamondi.
Naye beki wa Yanga, Ibrahim Hamad (Bacca), alisema wamejipanga vizuri na anayefanya vizuri katika dakika 90 ataondoka na alama tatu katika mchezo huo.
"Haitakuwa mechi rahisi na kila mmoja wetu anahitaji kupata alama muhimu, tunahitaji kuzitumia vizuri dakika 90, kupambana na kusaka ushindi. Tumeona ubora wa safu ya ushambuliaji wa wapinzani wetu na kama mabeki hatutakuwa tayari kuruhusu kufungwa kirahisi," alisema beki huyo.
Kwa upande wa Simba, Roberto Oliveira (Robertinho), amesema ameifanyia kazi safu yake ya ulinzi kwa lengo la kutofanya tena makosa yatakayowagharimu.
Robertinho aliweka wazi ameshabaini changamoto za safu yake ya ulinzi na amezifanyia kazi ili kutoruhusu mabao kirahisi katika kila mechi kama ilivyojitokeza kwenye michezo iliyopita.
“Tuna mechi ngumu sana mbele yetu, tumekuwa tukiruhusu mabao, tunapotangulia kupata ushindi, ukiangalia mechi ya Al Ahly zote mbili nyumbani na ugenini lakini mchezo wetu na Ihefu FC, tumeruhusu bao licha ya kushinda.
Wachezaji wangu wanatambua umuhimu wa mechi yetu ijayo na tunahitaji kupata matokeo mazuri, nafahamu ubora wa wapinzani wetu, jukumu langu kubwa ni kufanyia kazi changamoto za kikosi changu,” alisema Robertinho.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema wamejiandaa vizuri na kikosi kipo imara kutafuta alama tatu ambazo zinaenda kutengeneza tofauti katika msimamo wa ligi .
“Tunatakiwa kumaliza mbio za ubingwa mapema, kurahisisha kazi na kupunguza presha, tumeona Azam FC wameshajitoa kwenye mstari sasa tunataka kusaka ushindi mchezo wetu wa Jumapili.
Tayari wameshapoteza alama tatu na katika mchezo huu tunahitaji kupunguza tatu nyingine, wachezaji wanatambua umuhimu wa mchezo huu na kuhakikisha wanapambana kuwapa furaha mashabiki wetu,” alisema Ahmed.









