Wabunge wapingwa vigogo kunyongwa

06Nov 2023
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
Wabunge wapingwa vigogo kunyongwa
  • Ni kuhusu sheria vigogo ubadhirifu kunyongwa, wasomi, wanasiasa wawapa somo...

WASOMI na wachambuzi wa masuala ya siasa  wamekosoa mapendekezo ya wabunge kuhusu sheria ya kunyongwa au kukatwa vichwa viongozi wa serikali waliotajwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusika na ubadhirifu wa fedha za umma.

Mchambuzi wa Masuala ya Kiuchumi, Prof. Haji Semboja.

Pamoja na kukosoa, wametaka kufanyike maboresho ya mifumo iliyopo ili kuwapo na uwajibikaji.

Juzi, bungeni jijini Dodoma, baadhi ya wabunge walipendekeza kunyongwa au kukatwa vichwa kwa viongozi wa serikali, wakiwamo mawaziri na watumishi wa umma, waliotajwa kuhusika na ufujaji na ubadhirifu.

Wabunge hao walisema umefika muda mwafaka wa kuwasilishwa bungeni muswada na sheria ya kutekeleza jambo hilo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia ya udokozi wa fedha za umma.

Wakizungumza na Nipashe katika mahojiano maalum kuhusiana na mapendekezo hayo, wadau hao walisema kinachotakiwa kufanyika ni kufanya maboresho katika mifumo iliyopo ili kuwapo kwa uwajibikaji pindi ripoti za CAG zinapotoka.

Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema kauli zilizotolewa na wabunge ni maneno ya kisiasa na hayana maana na kwamba ubadhirifu utaondoka kwa kujenga taasisi imara.

Mchambuzi wa Masuala ya Kiuchumi, Prof. Haji Semboja, alisema ripoti ya CAG huwa inatoa maelekezo lakini tatizo kubwa ni hatua hizo hazifuatwi au kuangaliwa.

“Bunge ni chombo cha kisheria labda walazimishe sheria zilizopo sasa hivi zifanye kazi baada ya ripoti hizo kutoka. Sasa hivi tuna bahati ripoti zinatoka kwa wakati, zamani ilikuwa zinachelewa sana. Lakini kuwahi kwake kunatuonesha kwamba tuna matatizo katika jamii ambayo imeendelea na mifumo yake haiko sawa na hakuna haja kutengeneza sheria nyingi,’ alisema.

Prof. Semboja alisema jambo la msingi ni kuboreshwa kwa mifumo ambayo itasaidia kuondokana na tatizo hilo ambapo utaratibu upo na unaeleza nini kifanyike baada ya ripoti ya CAG kutoka.

Alisisitiza  kuwa mapendekezo ya wabunge kuhusu kuwapo kwa sheria ya kunyongwa ni ngumu endapo mifumo haitaboreshwa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Richard Mbunda, alisema ameshangazwa na mapendekezo ya wabunge japo inaonyesha wameumia. Alisema  wabunge wamezungumza waziwazi kwa kuashiria kuumia kuona vigogo wanatumia mali za umma wakijua hakuna watakachofanywa.

“Hili bunge limekuwa likibezwa sana kwa maana ya jinsi likiendesha mambo. Mara nyingi lilionekana halikuwa ni bunge la wananchi pengine waliokwenda katika hilo bunge walibebwa na utawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Kimsingi wameonekana ni wabunge dhaifu katika mabunge yote tangu mfumo wa vyama vingi ulivyoanza, wapinzani ni wachache ikilinganishwa na miaka mingine ndiyo maana nimeshangazwa na namna walivyozungumza katika hilo,” alisema.

Dk. Mbunda alisema mawazo yao ya kutunga sheria kwa ajili ya kuwashughulia hao ni sahihi, lakini wanatakiwa kujua hawawezi kuitunga kwa ajili ya kuadhibu makosa ambayo tayari yameshafanyika.

Mwanaharakati wa masuala ya kisiasa na kijamii, Bubelwa Kaiza, alisema pengine bunge halijui wajibu wake kwa kuwa lina uwezo wa kufanya uamuzi.

“CAG ni ofisa wa bunge anakagua kwa niaba ya bunge si kwa niaba ya serikali. CAG huwa anakagua serikali, utendaji wake, matumizi ya fedha, kazi na matokeo ya kazi anakagua kwa niaba ya bunge.

Kaiza alisema walitakiwa kuangalia sheria zinasemaje na mamlaka waliyonayo kwa mujibu wa Katiba ili wachukue hatua kwa kuwa mamlaka hiyo ni yao.