Gamondi hataki presha kwa wachezaji wako

02Nov 2023
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Gamondi hataki presha kwa wachezaji wako

ZIKIWA zimebaki siku nne tu kabla ya mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga, Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema hana shaka na wachezaji wake katika kutimiza majukumu yao kwenye mchezo huo na hataki kuwapa presha.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi.

Akizungumza, Gamondi, alisema anafahamu mchezo dhidi ya Simba ni tofauti na michezo mingine, lakini hataki kuwabebesha mzigo wa presha wachezaji wake badala yake anaendelea kuwapa mbinu zitakazowasaidia kufanya vizuri.

Alisema ameifuatilia Simba katika michezo mingi, hivyo anafahamu nini cha kuwapa wachezaji wake katika kukabiliana nao siku hiyo ya mchezo.

"Presha itoke kwa mashabiki labda, lakini mimi nauchukulia mchezo huu kama michezo mingine ingawa ni kweli ni mechi kubwa sana katika Ligi ya Tanzania, nataka wachezaji wangu wafanye kila wanachokifanya kila wakati kwenye michezo mingine, hii itasaidia kupunguza presha kwa wachezaji na kuwapa nafasi ya kutimiza majukumu yao," alisema Gamondi.

"Tunataka kushinda Jumapili hilo ndilo jambo la msingi, tulipoteza kwa penalti kwenye mchezo wetu wa Ngao ya Jamii, tunaendelea kujipanga na kuwapa wachezaji mbinu zitakazotusaidia kupata ushindi," alisema Gamondi.

Aidha, Kocha huyo raia wa Argentina, alisema anafurahishwa na namna wachezaji wake wanavyojituma mazoezini na haoni presha yoyote kwao.

"Naomba tu mashabiki wetu wanaendelea kutusapoti, naamini utakuwa mchezo mzuri, tutacheza katika ubora wetu na katika mipango yetu," alisema Gamondi.

Simba itakuwa mwenyeji wa Yanga kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Jumapili, Novemba 5 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa majira ya saa 11 jioni.

Kwa upande wa Kiungo wa Yanga, Mudathir Yahya, ametamba kuwa hawako tayari kuona wanapoteza  kwa mara nyingine tena kwenye mechi hiyo ya watani wa jadi.

Tangu msimu uliopita Yanga imepoteza mara mbili, ikiwamo mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Ngao ya Jamii uliyopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Simba walitwaa ubingwa huo kwa mikwaju ya penalti.

Akizungumza na Nipashe jana, Mudathir alisema baada ya mchezo wao na Singida Fountain Gate FC, Kocha Gamondi amefanyia kazi madhaifu yao na ubora wa Simba.

“Maandalizi yako vizuri, hatutakuwa tayari kuona tunaenda kupoteza huu mchezo kwa mara nyingine, tuko imara na mashabiki wajitokeze kusapoti timu ili iendeleze ushindani,” alisema kiungo huyo.

* Imeandikwa na Faustine Feliciane na Saada Akida