Ameweka wazi wachezaji atakaowapa nafasi leo huku akimulika zaidi mechi ijayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vipers FC ya Uganda.
Baada ya mchezo huo wa leo utakaopigwa saa 10:00 alasiri, Simba itaendelea na maandalizi yake ya mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vipers itakayopigwa Jumanne ijayo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Katika mchezo uliopigwa Uwanja wa St. Mary's nchini Uganda Jumamosi iliyopita, Simba ilishinda bao 1-0 shukrani kwa Henock Inonga, aliyeiwezesha kuvuna pointi tatu za kwanza baada ya michezo mitatu ya hatua hiyo ya makundi.
Akizungumza na Nipashe jana, Robertinho alisema wamejipanga kuhakikisha wanashinda dhidi ya African Sports ili kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam, ASFC.
Alisema siku zote malengo ya Simba ni kushinda kila taji la michuano wanayoshiriki na kwa hali hiyo wanahitaji kupata ushindi katika mchezo wa leo.
Kocha huyo raia wa Brazil, alisema leo wanategemea kuwatumia wachezaji ambao hawapati nafasi kubwa kikosini kwa kuwa wiki ijayo wana mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vipers.
"Tumejipanga kuhakikisha tunashinda mchezo wa kesho (leo) wa Kombe la Shirikisho dhidi ya African Sports, Simba ni timu kubwa na tunahitaji kushinda kila taji na tupo tayari.
"Tunategemea kuwatumia wachezaji ambao hawajapata nafasi kubwa kikosini kwa kuwa tuna mchezo wa marudiano nyumbani dhidi ya Vipers kwa hiyo tunaziangalia mechi zote,” alisema Robertinho.
Hata hivyo, kuelekea mchezo wa leo, Robertinho atalazimika kumkosa mshambuliaji, Kibu Denis, ambaye atakuwa nje kwa wiki moja kutokana na kupata majeraha katika mchezo uliopita wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vipers.
Kibu alipata maumivu ya mguu na baada ya vipimo daktari wa timu hiyo, Edwin Kagabo, amesema anahitaji kuwa nje kwa mudu wa wiki moja ili kupona kabisa, lakini Simba itaendelea kumkosa Augustine Okrah, ambaye ndiyo kwanza ameanza mazoezi mepesi chini ya uangalizi kabla ya kujiunga pamoja na wenzake.
"Kibu alipata maumivu katika mchezo uliopita dhidi ya Vipers, hayakuwa mabaya sana, lakini inabidi akae nje ya uwanja kwa muda wa wiki moja ili kupona kabisa," alisema Dk. Kagabo.
Kwa upande wa Kocha wa African Sports, Mussa Rashid, alisema ana waheshimu Simba lakini wamejiandaa vizuri kuonyesha ushindani mkubwa katika mchezo huo.
"Tunatambua mchezo utakuwa na ushindani mkubwa na malengo yetu makubwa yalikuwa ni kufika na kucheza hatua ya 16-bora ya Kombe la Shirikisho," alisema kocha huyo.










