Uhamiaji FC imeibuka na jumla ya alama sita katika michezo yake hiyo miwili ya mzunguko wa 21 na 22, hivyo kurejesha hamasa kwa mashabiki wake.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdi Salehe, alisema amekiimarisha kikosi chake ili kuhakikisha katika michezo hii ya mwisho wanafanya vizuri na kumaliza ligi katika nafasi nzuri.
Alisema kushinda michezo miwili mfululizo dhidi ya timu hizo kongwe katika soka la Zanzibar, kumemjengea matumaini ya kufanya vizuri hata kwenye michezo iliyobaki ili kutimiza lengo lao la kumaliza katika nafasi nne za juu.
Alisema anajua katika michezo iliyobaki itakuwa migumu zaidi kwa kuwa timu zinazogombania ubingwa zinahitaji kushinda ili kuhakikisha zinatimiza kiu yao huku na wao wakiendeleza mipango yao ya kuzoa alama katika michezo hiyo.
“Kushinda michezo miwili mfululizo katika hatua hii ya lala salama si jambo rahisi, kama tunavyojua mechi za mwisho za ligi zinakuwa ni za mapambano makali, kila timu inahitaji kutimiza lengo lake na kuna timu ambazo zinataka kushuka nazo ukikutana nazo zinakuja kwa kasi ili kupata matokeo yatakayowabakisha Ligi Kuu, hivyo lazima mipango yetu hii ya kufanya vizuri iwe endelevu hadi mwisho,” alisema kocha huyo ambaye timu yake sasa imefikisha alama 34 ikiwa nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu wenye timu 16.










