Yanga SC yatikisa kwa rekodi Ligi Kuu

02Mar 2023
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yanga SC yatikisa kwa rekodi Ligi Kuu

HUKU straika wake, Fiston Mayele, akiendelea kuongoza kwenye orodha ya wafungaji akiwa na mabao 15, timu ya Yanga imeendelea kujizolea rekodi lukuki za kufanya vema kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo kwa sasa inaongoza kwa kushinda mechi nyingi ugenini na nyumbani pia.

 

Mbali na rekodi hiyo, Yanga iliyopo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi 62, ndiyo timu iliyoshinda mechi nyingi zaidi za jumla, ikitoka sare mara chache zaidi na kufungwa mabao machache pia.

Kwa mujibu wa rekodi na takwimu za Ligi Kuu hadi kufikia raundi ya 24, Yanga imeshinda mechi 10 kati ya 11 za ugenini ikiwa na maana haijashinda mchezo mmoja tu kati ya hizo na hiyo ilikuwa ni Novemba 29, mwaka jana, ilipochapwa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu, katika Uwanja wa Highland, Estates, Mbarali mkoani Mbeya.

Simba inashika nafasi ya pili kwa timu zilizoshinda mechi nyingi ugenini, ikishinda mara saba kati ya mechi 12 ilizocheza hadi kufikia raundi hiyo.

Kwenye mechi tano ambazo imeshindwa kufanya kuibuka na ushindi nyumbani ni dhidi ya Azam FC ilipochapwa bao 1-0, sare ya bao 1-1 dhidi ya Wanalambalamba hao pia sare ya 1-1 dhidi ya Mbeya City, Yanga, Kagera Sugar na nyingine kwa Singida Big Stars.

Timu ya Singida Big Stars iko kwenye nafasi ya tatu kwa timu zilizoshinda mechi nyingi ugenini, ikicheza mechi 12 na kushinda tano, Azam ipo nafasi ya nne, ikishinda nne ugenini kwa michezo yake 12, huku Namungo ikiwa nafasi ya tano, ikishinda mechi nne, lakini ikicheza mechi 14 za ugenini mpaka sasa.

Kwenye mechi za ushindi wa nyumbani, Yanga imeshinda mechi 10 kati ya 12 ilizocheza, na michezo miwili ambayo ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Azam na 1-1 dhidi ya Simba.

Timu ya Azam inashika nafasi ya pili kwa kushinda mechi nyingi za nyumbani ambayo nayo kama Yanga imeshinda mechi 10 kati ya 12, lakini Wanalambalamba hao wako kwenye nafasi ya pili kwa sababu mechi zao mbili moja wamepoteza, tofauti ya wenzao ambao wametoka sare zote.

Azam ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Geita Gold nyumbani na kuchapwa mabao 3-2 dhidi ya Yanga.

Simba iko kwenye nafasi ya tatu kwa kwa kushinda mechi tisa nyumbani kati ya 11 ilizocheza huku Singida Big Stars ikiwa nafasi ya nne kwa kucheza mechi 12, ikishinda tisa.

Mabingwa watetezi, Yanga wanaongoza kwa kushinda mechi nyingi, ikifanya hivyo mara 20, ikifuatiwa na Simba mara 16, ikitoa sare mara mbili tu ambayo ni idadi ya chini zaidi kuliko timu yoyote, ikiruhusu mabao machache zaidi kwenye Ligi Kuu mpaka sasa, ambayo ni 10, ikifuatiwa na Simba iliyoruhusu wavu wake kutikiswa mara 14.