Ridhiwani Kikwete alia 'fitna' zilimuondoa Yanga

27Apr 2016
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Ridhiwani Kikwete alia 'fitna' zilimuondoa Yanga
  • ...Hadi jana hakuna barua rasmi kutoka Yanga aliyopokea ikimueleza amevuliwa uanachama tangu mwaka 2013 ilipotangazwa...

HUKU Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikitangaza uchaguzi mkuu wa klabu ya Yanga utafanyika Juni 5 mwaka huu, aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo,....

Ridhiwani Kikwete

Ridhiwani Kikwete amesema kwamba kufutwa kwake uanachama kulitokana na 'fitna' za baadhi ya viongozi ambao walikuwa hawataki kuambiwa ukweli.

Akizungumza na gazeti hili jana, Ridhiwani alisema kuwa baadhi ya viongozi walioko madarakani walikuwa hawataki kuambiwa ukweli wanapokea na badala yake waliwaona wanachama hao ni 'maadui'.

Ridhiwani alisema kwamba bado haamini kama yeye si mwanachama wa Yanga kwa sababu tu alikuwa akishinikiza kufanyika kwa uchaguzi mkuu kama katiba yao ilivyokuwa inasema baada ya muda wa viongozi kukaa madarakani kumalizika.

"Nilipiga kelele hadi (alitaja jina la kiongozi mmoja wa TFF) akawa ananinunia, 'figisu' za uchaguzi zilinifanya nikafutwa uanachama, nashangaa leo kusikia wanalazimishwa kufanya uchaguzi na BMT (Baraza la Michezo la Taifa), sasa timu itarudi kwa wazalendo," alisema Ridhiwani.

Hata hivyo Ridhiwani ambaye alijiunga na Yanga tangu mwaka 1996 hadi jana mchana alikuwa hajapewa barua yoyote ya kikao kilichoamua kumvua uanachama wa klabu hiyo zaidi ya kumsikia kwenye vyombo vya habari aliyekuwa msemaji, Baraka Kizuguto akitangaza.