Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa viongozi wa klabu hiyo wanatarajia kuwaacha wachezaji ambao hawana tija kwenye timu na kusajili watakaoibeba timu hiyo kwenda kwenye mafanikio.
Mmoja wa wajumbe wa klabu hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe kwa madai si msemaji na pia muda muafaka wa kuweka hewani hilo bado haijafika, alisema imefika muda sasa kusajili wachezaji wa kigeni wenye uwezo mkubwa wa kuisaidia timu na si kusaidia na klabu.
"Ninavyokwambia tuko kwenye mikakati mikali kwa ajili ya usajili wa msimu ujao wa ligi, tumechokwa kunyanyaswa na kusimangwa, tumeamua sasa tusimame kidete hasa kwenye usajili wa wachezaji wa kimataifa," alisema mjumbe huyo.
Ingawa alikataa kutaja wachezaji watakaoenda na maji, lakini mwanachama mmoja wa klabu hiyo alidokeza kuwa huenda watakaokumbwa na fyekafyeka hiyo ni Mrundi Emily Nimuboma, Waganda Hamisi Kiiza na Brian Majegwa, na Mkenya Paul Kiongera.
Wachezaji ambao wanaonekana bado wana msaada kwenye kikosi ni kipa kutoka Ivory Coast Vicent Angban, kiungo Mzimbabwe Justice Majabvi, na mganda Juuko Murshid.
Taarifa zinasema kuwa Kiiza anatarajiwa kuachwa baada ya msimu huu kutokana na kudaiwa kuwa amekuwa haisaidii timu inapokutana na mechi ngumu na muhimu, hasa dhidi ya Yanga pamoja na zile ambazo timu inahitaji matokeo kwa udi na uvumba.










