Kiwango Mwadui FC chamshangaza Hall

27Apr 2016
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Kiwango Mwadui FC chamshangaza Hall

BAADA ya kufanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho (FA) Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall amesema kuwa mchezo wao dhidi ya Mwadui FC ulikuwa mgumu na juhudi binafsi za wachezaji wake ziliwasaidia kupata ushindi.

Kocha wa Mwadui FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio akishangilia na wachezaji wake.:picha ya maktaba.

Azam FC imefanikiwa kutinga fainali baada ya kuifunga Mwadui FC penalti 5-3 kufuatia sare ya magoli 2-2 katika dakika 120.

Akizungumza na gazeti hili jana, Hall alisema mchezo huo dhidi ya kikosi hicho kinachonolewa na Jamhuri Kihwelu 'Julio' ulikuwa na changamoto mbalimbali kutokana na wachezaji wa timu zote kufahamiana na kuwa na uzoefu wa mechi za mtoano.

"Walituweka kwenye wakati mgumu, tulikuwa kwenye changamoto muda wote wa mchezo, ila nafurahi tumevuka hatua hii," alisema Hall.

Kocha huyo alisema kuwa mechi za mashindano hayo zimewasaidia wachezaji wake kuimarika na kuwaweka kwenye nafasi nzuri ya kuelekea kwenye mbio za kusaka ubingwa wa Bara.

Azam FC sasa inasubiri uamuzi wa Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuhusiana na mchezo mwingine wa nusu fainali uliovunjika kati ya Coastal Union na Yanga iliyokuwa mbele kwa mabao 2-1.