Real Madrid waliwafunga majirani zao Atletico Madrid mabao 4-1 na kutwaa taji la 10 - Klabu Bingwa Ulaya.
Sasa wanakutana tena katika fainali inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka duniani kote.
Miaka kadhaa nyuma, Real Madrid ilikuwa na nafasi kubwa ya kuifunga Atletico kila walipokuwa wakikutana.
Lakini sasa, timu hizo zinakutana katika ubora tofauti, huku Madrid wakiongeza kiwango chao uwanjani tangu kuondoka kwa Rafa Benitez na nafasi yake kuchukuliwa na Zinedine Zidane, ambaye atakuwa akijaribu kutwaa taji kubwa Ulaya katika msimu wake wa kwanza kufundisha.
Majirani hao wanakutana katika mechi ya 54, Real Madrid wakishinda 31, Atletico 9 na sare 14.
Lakini tangu Real Madrid walipotwaa taji la Ulaya msimu wa 2013/14, wameweza kuifunga Atletico mchezo mmoja tu kati ya 10 waliyokutana.
Mshambuliaji wa Real, Cristiano Ronaldo amefunga mabao 16 kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na anahitaji mabao mawili ili kuvunja rekodi yake mwenyewe ya kufunga mabao 17 katika msimu waliotwaa taji mara ya mwisho 2013/14.
Zidane alikuwa shujaa wa Los Blancos kwa kufunga bao muhimu kwenye fainali ya msimu wa 2001/02 dhidi ya Bayer Leverkusen.
Sasa atashuka dimbani kuiongoza Real kutwaa ubingwa, lakini nyuma yake akisaka rekodi binafsi ya kuwa mtu wa saba kushinda taji kubwa la Uefa akiwa kama mchezaji na kocha.
Wapinzani wao, Atletico Madrid watakuwa wakijaribu kutwaa taji kwa mara ya kwanza, lakini nyuma yake pia wakitaka kulipa kisasi cha kufungwa katika mechi ya fainali miaka miwili iliyopita mjini, Lisbon Ureno.
Kocha Diego Simeone, aliwahi kusema kuwa timu yake Atletico Madrid imeziondoa kwenye mashindano timu mbili kubwa za daraja la kwanza kwa ubora duniani - Barcelona na Bayern Munich kuelekea kutwaa taji dhidi ya Real.
Winga wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo aliumia mguu mwanzoni mwa wiki hii wakati wa mazoezi ya kujiandaa na mechi hiyo.
Pamoja na kuwapo na ushahidi wa nyota huyo wa Ureno kutokuwa fiti kwa asilimia 100 kucheza mechi hiyo, lakini ataanza kwenye kikosi cha kwanza cha Zidane.
Kikosi cha Simeone hakina mchezaji yeyote majeruhi na atakabiliwa na wakati mgumu kupanga kikosi cha kwanza, kwani wachezaji wake wote wameonyesha kiu ya kutaka kuanza mchezo huo.
Kikosi kinachoweza kuanza kwa Atletico Madrid inayotumia mfumo wa 4-4-2 ni;
Oblak – Felipe Luis, Godin, Gimenez, Juanfran – Carrasco, Gabi, Koke, Niguez – Torres, Griezmann.
Real Madrid wanaotumia mfumo wa 4-3-3, huenda timu ikaanza hivi; Navas – Marcelo, Pepe, Ramos, Carvajal – Kroos, Casemiro, Modric – Bale, Benzema, Ronaldo.










