Yanga imetinga raundi ya kwanza ya michuano hiyo ikiing'oa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0 wakati APR iliyoanza kwa kichapo ugenini, ikisonga mbele kwa jumla ya magoli 4-2.
Pluijm alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa mashindano hayo yana changamoto nyingi kadri timu zinapotoka hatua moja kwenda nyingine, lakini 'Yanga imejipanga kukabiliana na hali hiyo'.
Mdachi huyo alitamba kuwa kikosi chake msimu huu kina wachezaji wenye uzoefu wa mashindano ya kimataifa na anaamini malengo yao ya kufika hatua ya makundi yatatimia.
"Yanga iko tayari kucheza na timu yoyote, hatuna hofu, siyo kwa klabu hiyo ya Rwanda (APR), tulivyofuzu kucheza mashindano haya ya Caf, tulikuwa tayari kupambana na yoyote," alisema Pluijm.
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' alisema mechi yao dhidi ya APR itakuwa ngumu kutokana na kujuana kwa wachezaji wa timu hizo mbili.
Kikosi cha Yanga sasa kinajiandaa kuikabili Azam FC katika mchezo wa raundi ya 21 ya Ligi Kuu Tanzania Bara utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi.










