Simba ambayo haijatwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa miaka minne, juzi ilishinda 5-1 dhidi ya timu hiyo ya Ligi Daraja la Pili (SDL) kwenye Uwanja wa Taifa na kutinga robo-fainali ya Kombe la Shirikisho.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mechi hiyo ya ushindi mnono, Mayanja alisema wachezaji wamekuwa wakimuelewa kwa haraka na kufuata maelekezo yake, kitu ambacho kinampa matumaini ya kufanya vizuri katika mechi zijazo.
"Inafurahisha kuona unawatuma wachezaji na wanafuata maelekezo yako kwa vitendo, vijana wanafanya kazi kubwa na dhamira ya ubingwa msimu huu ipo palepale," alisema Mayanja.
Kocha wa Singida United, Fulgence Novatus, alisema Simba ni timu kubwa na imewapa somo tosha kukisuka upya kikosi chao ili kifanye vizuri msimu ujao ambao watakuwa wanashiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
"Simba ilikuwa ni mfupa mgumu kwetu ila tumejifunza kutoka kwao, tutafanyia kazi dosari zilizojitokeza. Vijana wetu wana uchu wa mafanikio," alisema Flugence.










