Mechi hiyo ya hatua ya 16-bora ya michuano hiyo, itakuwa ya kwanza kwa Azam FC kucheza mjini Moshi kutokana na mkoa wa Kilimanjaro kutokuwa na timu Ligi Kuu tangu kikosi cha Wanalambalamba kianze kushiriki Ligi Kuu msimu wa 2008/09.
Baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), kocha wa timu hiyo ya Chamazi, Stewart Hall, alisema wamefuata ushindi katika mechi hiyo huku akiweka wazi kuwa amepanga kumtumia straika wake, Didier Kavumbagu aliyekuwa nje ya uwanja kwa miezi miwili kutokana na majeraha ya enka.
"Tumekuja hapa kushinda kwa sababu tunautaka ubingwa wa FA, maandalizi yetu tayari yamekamilika," alisema. "Tumekuja na kikosi imara chenye wachezaji 22. Ni jambo jema kuona Kavumbagu yupo 'fiti' na yupo katika mipango ya mechi hiyo.
"Tumeamua kuweka kambi Arusha baada ya kukosa hoteli ndani ya mji wa Moshi, ninafikiri imetokana na mashindano ya Kilimanjaro Marathon, kuna wageni wengi hivi sasa Moshi ikizingatiwa ni mji mdogo.
“Tunatarajia uwanja tutakaochezea utakuwa mbovu, mimi sijauona, ila nimepata ripoti, pia hatujapata nafasi ya kufanya mazoezi kwenye uwanja huo siku moja kabla ya mechi kama inavyotakiwa kutokana na Kilimanjaro Marathon, hili ni tatizo kwetu.”
Azam FC ilifuzu kwa hatua hiyo baada ya kuichapa African Lyon mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam, shukrani kwa mabao ya Farid Mussa, aliyefunga mawili huku Mudathir Yahya na Ame Ally wakitupia moja kila mmoja.
Panone FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL) na kufundishwa na kocha wa zamani wa Yanga (Minziro), iliitoa timu ya Madini ya mkoani Arusha kwa mabao 3-1 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Ushirika.
Mshindi wa mchezo huo atafuzu moja kwa moja kwa hatua ya robo-fainali ya michuano hiyo ambayo bingwa wake atawakilishi wa Tanzania Bara kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mwakani.










