Pluijm: Sikutegemea, Yanga wataikoma

01Feb 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Pluijm: Sikutegemea, Yanga wataikoma
  • * Yanga imepoteza mechi yake kwanza Ligi Kuu Bara msimu huu kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga... Kocha Hans van Der Pluijm wa Yanga.

Coastal Union ya Tanga juzi ilivunja utamaduni wa muda mrefu wa mashabiki wa Yanga kundoka uwanjani bila kuinamisha vichwa baada ya kuwachapa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Kama ambavyo wapenzi na mashabiki wa Yanga kutotarajia kisago hicho cha kwanza msimu huu, ndivyo pia ilivyokuwa kwa bosi Hans van der Pluijm.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu kuhusu mchezo huo, Kocha Pluijm alisema neno moja tu: "Sikutegemea."

Alisema uimara wa kikosi chake kulinganisha na wapinzani wao, ndiyo unamfanya kushindwa kuamini matokeo hayo.
Hii ni mara ya kwanza kwa Yanga kupoteza mechi ya Ligi Kuu Bara tangu ilipoachia pointi tangu Mei mwaka jana baada ya kufungwa na Ndanda ya Mtwara.

"Sikutegemea matokeo haya, yamenishangaza, lakini mpira ndivyo ulivyo," alisema.
"Hatuangalii nyuma, tunasahau yaliyotokea nyuma, tutaka kurekebisha makosa na kupata ushindi wenye mechi zinazofuata."

Alisema kwa tathmini, kikosi chake kilicheza vizuri na ndicho kilichostahili kushinda mechi hiyo.

"Ni kama vile hatukuwa na bahati, tulitengeeza nafasi nyingi za kushinda tukashindwa kuzitumia," alisema kocha hiyo wakati akilizungumzia pambano hilo lililochezeshwa na mwamuzi kwa zaidi ya dakika 100 na kuzaa kadi mbili nyekundu.

Alisema kilichoiponza Yanga ni ukosefu wa umakini na kwamba wapinzani wao walitumia vizuri nafasi chache walizopata.
"Safu ya ulinzi haikuwa makini, waliwaruhusu Coastal Union kufanya mashambulizi mara kwa mara, hii siyo kawaida ya Yanga."

Winga machachari wa timu hiyo, Simon Msuva alisema jana kuwa wachezaji wameumia kupoteza mechi hiyo lakini hawawezi kukwepa kilichotokea.

Mabao ya Union yalifungwa na Miraj Adam kwa shuti la adhabu ndogo kutoka nje ya 18 na kupenya katikati ya miguu ya kipa Dida, kabla ya Juma Mahadhi kuhakikisha ushindi kwa kufunga bao la pili kwa shuti kali nje ya eneo la hatari.

Pamoja na kupoteza mchezo huo, mabingwa Yanga bado wanaongoza msimamo wa ligi kwa kuwa na pointi 39, sawa na Azam wanaoshika nafasi ya pili.