Bayi: Pelekeni mabondia wenye viwango Olimpiki

30Jan 2016
Nipashe
Bayi: Pelekeni mabondia wenye viwango Olimpiki

KAMATI ya Olimpiki Tanzania (TOC) imelitaka Shirikisho la Ngumi za Ridhaa (BFT) kuhakikisha linapeleka wachezaji wenye uwezo katika mashindano ya kusaka viwango vya kufuzu kushiriki michezo ijayo olimpiki.

Katibu wa TOC, Filbert Bayi

Michezo ya Olimpiki 2016 itaanza rasmi Agosti 5 Rio de Jenairo, Brazil.
Katibu wa TOC, Filbert Bayi, alisema jana kuwa BFT inapaswa kuangalia na kupeleka Cameroon mabondia wenye uwezo ambao baada ya kufuzu, wataiwakilisha vyema Tanzania nchini Brazil.
Bayi alisema shirikisho hilo linapaswa kukumbuka ya kuwa mashindano ya Cameroon ndiyo ya mwisho kwao kwa ajili ya kusaka viwango, na ikiwa watashindwa, mchezo wa ngumi utakosa mwakilishi katika michezo hiyo ya kimataifa inayofanyika kila baada ya miaka minne.
"Kocha na viongozi wanapaswa kuchagua mabondia wenye uwezo ambao wana uhakika watafanya vizuri na kupata viwango vitakavyowawezesha kuiwakilisha nchi katika mashindano hayo," alisema Bayi.
Makore Mashaga, Katibu wa BFT, alisema ja kuwa mabondia watakaochaguliwa kwenda Cameroon, ni wale watakaofanya vizuri katika mashindano ya Taifa ya ngumi za ridhaa yaliyopangwa kufanyika Februari 6 kwenye Viwanja vya Tanganyika Packers.