Imeelezwa kuwa tukio hilo lilitokea baada ya mchezo huo wa kwanza wa duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara kumalizika wakati Twalibu na wanachama wengine wa Yanga walipoanza kutoa shutuma kwa benchi la ufundi la timu hiyo kutokana na kipigo hicho.
Twalibu aliiambia Nipashe jana kuwa baada ya timu yao kufungwa goli la pili, mashabiki wengi walianza kuwapigia kelele watendaji wa benchi la ufundi.
"Mpira ulivyoisha Muro aliniita na nikakataa, akaenda kuwaambia askari polisi wanikamate, lakini alipoona sijakamatwa akaenda kwenye Harrier yake (gari lake) akatoa bastola na kunitishia kunipiga nayo," alisema Twalibu.
Alidai kuwa Muro hakuishia hapo kwani alimfuata mpaka kwenye hoteli waliyofikia mashabiki wengi wa klabu hiyo waliotoka Dar es Salaam na kumtishia tena kumpiga kwa chombo hicho cha moto.
"Nilivyoona hivyo, nilienda kwenye kituo cha Polisi cha Pangani na nimetoa maelezo yangu na kuandikiwa RB," alisema Twalibu.
Aidha, alisema amefungua malalamiko kwenye kituo hicho ya 'kutishiwa kupigwa risasi' na kupewa RB namba Tan/RB/0662/2016.
Alipotafutwa na gazeti hili jana kuzungumzia tuhuma hizo, Muro alikana na kudai kuwa ni "uzushi tu".
"Duuh, mimi hata sijaja na bastola Tanga, Twalibu alimpiga ngumi na kumpasua kijana mmoja shabiki wa Yanga tawi la Manzese, sasa watu wakawa wanamwambia (Twalib) kwamba Jerry akikushika, atakupiga bastola, ni maneno tu ya watu mimi sijafanya hivyo," aliema Muro.









