Singida Fountain Gate FC inakuwa klabu ya pili inayoshiriki ligi hiyo kunufaika na mpango huo unaohusisha mkopo nafuu kutoka benki hiyo baada ya Klabu ya KMC ya kinondoni kunufaika na mpango kama huo mwezi Februari mwaka huu.
Hafla ya makabidhiano ya basi hilo lenye thamani ya sh ya milioni 470 imefanyika jana kwenye Uwanja wa CCM Liti, mkoani Singida ikihusisha viongozi waaandamizi wa benki ya NBC wakiongozwa na Mkurugenzi wa Biashara wa benki hiyo, Elvis Ndunguru sambamba na Rais wa Klabu hiyo Japhet Makau, ikienda sambamba na shamramshara za maadhimisho ya siku ya Singida Big Day zilizofanyika viwanjani hapo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Ndunguru alisema basi hilo ni sehemu ya mpango wa utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa vilabu vinavyoshiriki ligi hiyo ambapo klabu ya Singida Fountain Gate FC inatakiwa kurejesha mkopo huo ndani ya miaka miwili ukiwa na riba shindani katika soko.
‘’Basi hili ni ‘brand new’ la mwaka 2023, na limekatiwa bima na Benki ya NBC ambayo ina cover usalama wa abiria wote ndani ya gari na bima inatumika kwa nchi za Africa Mashariki na kati (Comesa). Gari limenunuliwa toka kampuni ya Africarriers Co. Ltd ya jijini Dar likiwa na uwezo wa kubeba abiria 58,’’ alifafanua Ndunguru.
Kwa mujibu wa Ndunguru ukosefu wa vyombo vya usafiri maalum kwa ajili ya timu zinazoshiriki ligi hiyo imekua ni moja ya chanzo cha vikwazo vingi katika gharama za uendeshaji na utendaji wa timu husika.
“Zaidi pia NBC tunaendelea kushirikiana kampuni washirika wa huduma za Bima wa Sanlam na Britam inatoa huduma za bima za afya na maisha kwa wachezaji wote wa timu zinashiriki ligi kuu ya NBC , mabenchi ya ufundi pamoja na familia zao.’’ aliongeza.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Rais wa Klabu hiyo Japhet Makau pamoja kuishukuru benki hiyo kwa hatua hiyo kwa jitihada zake za kuiboresha ligi hiyo kimataifa alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha kwamba mkopo huo unarejeshwa kwa wakati huku pia akiahidi kulitunza vyema basi hilo.
“Kupitia usafiri huu sasa tuna uhakika wa kusafirisha wachezaji wote na benchi la ufundi sambamba na mashabiki zaidi kwenda kwenye mechi zetu nje ya mkoa. Tunahidi kurejesha mkopo huu ndani ya muda unaotakiwa kama tulivyokubalina na NBC’’ alisema.










