Mo Dewji hana shida, wanachama ndio tatizo -FCC

04Aug 2023
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Mo Dewji hana shida, wanachama ndio tatizo -FCC
  • Yaeleza mwekezaji amekamilisha taratibu alizotakiwa kuzikamilisha, tatizo lipo upande wa....

TUME ya Ushindani wa Biashara (FCC), imesema suala la uwekezaji wa klabu ya Simba tatizo lipo kwa upande wa wanachama wa klabu hiyo na si muwekezaji Mohamed Dewji ‘Mo’.

Tume hiyo ilisema kila upande ulipewa majukumu kwa ajili ya kukamilisha mchakato huo na mwekezaji amekamilisha kwa upande wake lakini upande wa mashabiki umekwama.

Akizungumza jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio alisema anashangazwa na kinachozungumzwa sasa kwenye vyombo vya habari kuwa mwekezaji amekwamisha uwekezaji huo.

Alisema mwekezaji kwa upande wake alitekeleza kile alichotakiwa kufanya kukamilisha mchakato huo na upande wa wanachama nao walipewa mambo ya kuyakamilisha lakini mpaka sasa wameshindwa.

“Nakumbuka wiki mbili zilizopita nilipata barua kutoka RITA (Wakala wa usajili, Ufilisi na Udhamini) walikuwa wamewaita Simba upande wa klabu, siyo upande wa mwekezaji kwa sababu kwenye mkataba kulikuwa na majukumu ya mwekezaji na yale ya klabu kuweka sawa kuelekea katika Simba Sports Club Limited, mwekezaji ana ya kwake na hawa wengine kwa upande wa wanachama wanatakiwa kuweka hati ya jengo la klabu na mali nyingine, vyote hivi vinatakiwa vitoke mikononi mwa klabu na viende mikononi mwa Simba Sports Club Limited, walikuwa wameitwa RITA kwa ajili ya kuendelea kukamilisha hilo zoezi,” alisema Mkurugenzi Mkuu huyo.

Alisema katika makubaliano hayo kila upande unatakiwa kukamilisha majukumu ambayo waliagizwa kuyafanya ili mchakato ukamilike.

“Sijafuatilia nini kilitokea baada ya hapo lakini nilipata taarifa kuwa upande wa klabu uliitwa kwenda kuhakikisha, kuambiwa makubaliano yale yana pande mbili kuna upande mmoja chini ya Baraza la Wadhamini halafu upande wa pili ni wa Mwekezaji, wote wana kitu cha kufanya katika hili, bahati mbaya sana kinachozungumzwa sana kwenye vyombo vya habari ni yale majukumu ya mwekezaji na hakuna anayeangalia katika hili Simba nao wanatakiwa wafanye nini lakini katika hicho wanachotakiwa kufanya kama Baraza la wadhamini nalo linaendelea kushughulikiwa, mwekezaji kwa upande wake alishafanya kile anachotakiwa kukifanya na kilibaki upande wa klabu”, alisema.

Alisema kwa upande wao kama FCC walishalifunga jambo hilo kwa kuwa wali likamilisha kwa kubariki mchakato huo na kuwapa masharti na majukumu ya kufanya, hivyo suala hilo kwao lilishaondoka.

“Sisi na Simba suala letu tulilifunga kwa sababu walikuja wakapewa masharti, kuna majukumu yaliyokuwa ya mwekezaji na majukumu yaliyokuwa ya Simba yenyewe, sasa ilipoletwa baada ya vigezo kukamilika tulitoa cheti cha ruhusa kuwa muungano ule umepitishwa kile kilichokuwa kimeombwa kimeridhiwa baada ya hapo kilichobaki kwao ni utekelezaji tu,” alisema Erio.

Aidha, alipotafutwa Mwenyekiti wa klabu ya Simba ambaye anaingia kwenye vikao vya bodi ya klabu hiyo akiwakilisha upande wa wanachama, alisema FCC wako sahihi kueleza wapi mchakato huu ulipokwamia na wametusaidia sisi kufahamu.

“Nadhani katika hili watafuteni wazee wa Baraza la Wadhamini wao wanaweza kukwambieni zaidi tatizo ni nini, mimi binafsi sina la kuongea, FCC wameshawaambieni hivyo,” alisema Mangungu.

Mchakato wa mabadiliko ndani ya klabu ya Simba ulioanza mwaka 2017 umeonekana kuchukua muda mrefu na mara kwa mara kumekuwa kunaibuka sintofahamu, huku wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wakiwa hawajui haswa ni kitu gani, wapi au nani anakwambisha mchakato huo usikamilike.