Mayanja aanika ya Kerr Simba

10Feb 2016
WAANDISHI WETU
Lete Raha
Mayanja aanika ya Kerr Simba

KOCHA Jackson Mayanja amefunguka kuhusu mafanikio yake Simba na kilichoiyumbisha klabu hiyo chini ya Muingereza Dylan Kerr aliyetimuliwa.

Kocha Jackson Mayanja

Kabla ya kutimuliwa Simba, Kerr alikuwa akilalamikia mara kwa mara kuwa viwango vya mastraika wa timu hiyo ni tatizo, lakini imefichuka kuwa tatizo lilikuwa ni lake mwenyewe.Tangu alipowasili Mayanja, mastraika wa Simba waliokuwa wanaonekana mzigo, wamebadilika na kuwa moto wa kuotea mbali ndani ya kipindi kifupi.Kerr aliiongoza Simba kwenye mechi 13 za ligi msimu huu akishinda nane, sare tatu na vipigo viwili, wakidondosha jumla ya pointi 12. Simba chini ya Mayanja imecheza mechi tano, wameshinda zote na kujikusanyia pointi 15 huku timu yake ikifunga jumla ya mabao 13 na kuruhusu moja tu.Hata hivyo, Kerr alianzia mikoani na takwimu zinaonyesha kuwa Simba na Yanga hazijaweza kufunga zaidi ya mabao mawili nje ya jiji la Dar es Salaam kufikia sasa msimu huu.Kwenye mechi 13 za Kerr Msimbazi, mechi saba walicheza ugenini nje ya Dar es Salaam wakati mechi sita alicheza kwenye uwanja wa Taifa. Mayanja ametengeneza rekodi nzuri ambayo ni wastani wa mabao matatu kwa kila mechi.MIFUMO YA KERR Kuhusu lawama za Kerr kwa mastraika wa Simba, Mayanja amesema kilichokuwa kikiwaathiri ni mifumo iliyokuwa haiendani na wachezaji waliopo.Mayanja alisema, “Hakuna straika ambaye ninaona ni mzigo ndani ya kikosi changu, kila mmoja anafanya kile ninachomwelekeza na ndiyo maana wanafunga mabao.Kikubwa nilichokifanya niliwasoma na nikaanza kutumia mifumo ambayo inaendana na uwezo na kasi zao.“Pengine alichokuwa anakosea Kerr ni mifumo, kwa staili yake alikuwa akitoa nafasi kwa straika mmoja huku akijaza viungo wengi kati.“Kilichokuwa kinatokea ni kuwa pasi zilikuwa zikipigwa nyingi katikati ya uwanja, lakini timu ikawa inakosa madhara inapoenda mbele kwani mmaliziaji alikuwa mmoja.“Mimi ninatengenezea mazingira washambuliaji kwa mfumo ambao unawawezesha wachezaji watano kuingia ndani ya eneo la kipa (eneo la 18) na hata wanapopoteza mpira kuna mfumo ninaotumia ili waweze kurudi kusaidia ulinzi,” alifafanua.Katika uongozi wake Kerr alitumia zaidi mfumo wa 4-5-1 unaoundwa na mabeki wanne, viungo watano (viungo wakabaji watatu na viungo washambuliaji wawili) na mshambuliaji mmoja. Wakati Mayanja anatumia zaidi 4-4-2, 4-3-3 na 4-2-4. Mayanja amesema anatumia 4-4-2 yenye mabeki wanne, viungo wanne (mkabaji mmoja) na washambuliaji wawili. 4-3-3 anacheza kwa kutegemea mabeki wanne, viungo watatu (wakabaji wawili) na washambuliaji watatu wenye kasi na ubunifu. Alisema 4-2-4 ni mfumo unaotumika wakati wa kushambulia. Hapa kunakuwa na mabeki wanne, viungo wawili na washambuliaji wanne.