Yanga itawavaa Cercle De Joachim ya nchini humo katika mechi yao ya kwanza ya hatua ya awali wa Klabu Bingwa Afrika na itajichimbia huko kwa ajili ya kuwakabili mahasimu wao wa Ligi Kuu ya Bara, Simba.
Nyota hao 21 watakuwa chini ya viongozi wa saba wa benchi la ufundi pamoja na mkuu wa msafara, Ayoub Nyenzi, kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF.
Kuelekea mchezo huo, Yanga imewaacha wachezaji watatu ambao ni winga Geofrey Mwashiuya na kipa Benedict Tinoco ambao hati zao za kusafiria hazikuwa tayari, wakati straika Matheo Anthony, ameachwa kwa kuwa hayuko fiti kimchezo.
Yanga imepanga kutumia safari hiyo kwaajili ya kuweka kambi kabla ya kuwakabili Simba Jumamosi wiki ijayo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, alisema kuwa mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Yanga hakitarejea moja kwa moja nchini bali kitaendelea kujifua kwaajili ya mechi yake ya Ligi Kuu dhidi ya Simba.
Kocha Hans van der Pluijm alisema timu yake imejiandaa vizuri kwa ajili ya ushindi na kwamba wachezaji wake wamekuwa wakielewa kile anachowapa mazoezini.
“Tupo tayari kwa ushindi, wachezaji wangu wako fiti na nidhamu yao pia ipo juu. Nimekuwa nikiifuatilia timu ya Cercle na inaonekana kuwa ni timu ambaayo tunaweza kuifunga.
“Sitaki kuwabeza, lakini nitaipeleka timu yangu ikacheze na kushinda. Tutakachokifanya ni kutafuta goli la mapema na kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu ili tusipate matatizo yoyote,” alisema kocha huyo.
Pluijm pia alisema kuwa ana uhakika wa kufika mbali kwenye michuano hiyo, kwa madai kuwa kama alitolewa kwenye Klabu Bingwa kwa bao moja la Etoile Du Sahel ya Tunisia kisha timu hiyo ikatwaa ubingwa wa michuano hiyo, kwanini Yanga ishindwe kufika mbali.
ANAVYOIPIGIA HESABU SIMBA
Mholanzi huyo alisema, “Sitaki nifikirie sana mchezo wa Simba, kwasasa ninaangalia jinsi gani nitaiwezesha timu yangu kufika mbali kwenye michuano ya kimataifa, lakini lengo langu ni kushinda kila mchezo unaaokuja mbele yetu.
“Baada ya kumaliza mchezo wa klabu bingwa, timu itaendelea kuwapo nchini Mauritius kwaajili ya kujiandaa na michezo ijayo ya ligi hasa ule dhidi ya Simba ambao uko mbele yetu.”
Mchezo wa Yanga dhidi ya Cercle De Joachim umepangwa kuchezwa Jumamosi hii (Februari 13) saa 9:30 alasiri kwa saa za Mauritius (sawa na saa 8:30 mchana kwa saa za Tanzania).









