Mama wa rais TFF ya Hispania agoma kula

31Aug 2023
Nipashe
Mama wa rais TFF ya Hispania agoma kula

MAMA mzazi wa rais wa Shirikisho la Soka la Hispania (RFEF), Luis Rubiales, amejifungia kanisani na kusema yuko kwenye mgomo wa kula akipinga namna mwanawe anavyoshinikizwa kujiuzulu, binamu wa Rubiales ameiambia ESPN.

Angeles Bejar alijifungia ndani ya kanisa la Divine Shepherdess katika mji wa nyumbani wa Rubiales wa Motril, Andalusia kuanzia Jumatatu.

Alisema ameamua kufanya mgomo huo kwa sababu ya mwanawe kushutumiwa kwa kosa ambalo halina ukweli wowote.

Rubiales amesimamishwa kwa muda wa siku 90 kujihusisha na masuala ya soka na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Ijumaa wakati Baraza Kuu la Michezo la Hispania pia linataka kumwondoa madarakani, kutokana na kumbusu mdomoni mchezaji wa Timu ya Taifa ya Wanawake, Jenni Hermoso.

Rais huyo alifanya hivyo baada ya Hispania kushinda Kombe la Dunia la Wanawake kwenye fainali iliyopigwa nchini Australia dhidi ya England.

Rubiales amekataa kujiuzulu kutokana na suala hilo, akisisitiza kwamba busu hilo lilikuwa la ridhaa - dai lililokataliwa na mchezaji huyo - na kutishia hatua za kisheria dhidi ya Hermoso.

Waendesha mashtaka wa Hispania walisema wamefungua uchunguzi wa awali wa unyanyasaji wa kijinsia katika tukio hilo.

Bejar aliiambia EFE mgomo wake utaendelea “kwa muda usiojulikana, mchana na usiku”.