Mashabiki wa Simba walikuwa wakipaza sauti mitandaoni na katika baadhi ya mechi wakisikika wakilalamika kitendo cha straika huyo aliyemaliza msimu uliopita akiwa na mabao 10 kabla ya kuumia, kutopewa nafasi na Kocha Mkuu, Robertinho Oliveira, huku baadhi ya vyombo vya habari (si Nipashe), vikidai hana maelewano na viongozi jambo ambalo umetoa maagizo kwa kocha kutompa nafasi.
Lakini straika huyo kipenzi cha mashabiki wa Simba, ameibuka na kusema hana tatizo lolote na kocha mkuu wa timu hiyo, Robertinho na kwamba kutopata nafasi ya kucheza kwake kumesababishwa na kukaa nje akiuguza majeraha kwa muda mrefu huku akisisitiza kuwa hafikirii kuondoka ndani ya timu hiyo kwa sasa.
Phiri alisema hakuna ukweli juu ya kutaka kuondoka ndani ya kikosi cha timu hiyo na kuweka wazi ataendelea kusalia ndani ya klabu hiyo na kwamba hana matatizo na Robertinho licha ya yeye kukosa nafasi ya kucheza kwa muda mrefu ndani ya timu hiyo.
“Bado nipo sana Simba, nina mkataba nao hakuna ukweli kuwa nataka kuondoka hapa, ninafura
ha na timu yangu na nitaendelea kupigania klabu yangu kila mechi kuhakikisha tunapata kile wanachokitarajia.”
“Nashindwa kupata nafasi ya kucheza kwa sababu ya kutoka katika majeraha ambayo yaliniweka nje kwa muda mrefu, napewa muda mdogo ili kuweza kurudi taratibu kuweza kupambana hakuna kitu kingine,” alisema Phiri.
Aliwaahidi mashabiki kupambania Simba kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na kufikia malengo yao ya kutwaa mataji likiwamo la Ligi Kuu, Kombe la FA na kuvuka robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, kuhusu sakata hilo la Phiri, naye alikanusha taarifa za mshambuliaji kutaka kuondoka kutokana na madai kwamba hana furaha ndani ya kikosi cha timu hiyo baada ya kutopata nafasi chini ya Robertinho.
Aliwataka mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kuachana na maneno yatakayowavuruga na kuwakosanisha na viongozi, wachezaji na benchi la ufundi.
“Phiri ni mchezaji halali wa Simba hakuna ukweli wowote kuhusu kutaka kuondoka, Wanasimba wanatakiwa kutulia kuwapa muda viongozi, benchi la ufundi na wachezaji ili kutengeneza timu kuwa imara.
Alisema kulingana na usajili waliofanya kwa wachezaji wengi wapya wanatakiwa kupata muda wa kuzoea mazingira na kuingia kwenye mfumo wa kocha Robertinho.
“Sasa tuna mashindano mengi mbele yetu, ikiwamo Super League ambayo Tanzania tutazindua mashindano hayo, tunatakiwa kupata sapoti kwa mashabiki wetu na kuachana na maneno ya watu wasioitakia mema Simba,” alisema Try Again.
Aidha, Try Again, alisema malengo yao makubwa ni kutwaa mataji yote ya ndani wanayoshiriki ikiwamo Ligi Kuu Tanzania Bara, kuvuka robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kufanya vizuri katika michuano ya Super League ndiyo maana walifanya usajili mkubwa kwa malengo.
Simba tayari imefanikiwa kutwaa taji la Ngao ya Jamii kwa ushindi wa penalti 3-1 dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga, mchezo uliopigwa Agosti 13,
mwaka huu, Mkwakwani jinini Tanga.
Try Again alisema: “Kama bodi, Simba tulikaa chini, tukaangalia malengo yetu ya mwaka huu kutwaa ubingwa na kuvuka robo fainali, tunafikaje huko. Lazima uwe na nyezo katika mpira maana yake ni wachezaji na benchi la ufundi.
“Tumesajili wachezaji wengi wenye ubora na hizi sio hasira ila tumesajili kwa ajili ya mahitaji ya timu yetu ili kufikia malengo hayo ambayo hata mashabiki na wapezi wa Simba wanayatarajia,” alisema Try Again.
Kuhusu usajili wa kiungo Frabrice Ngoma, kuwa wamemsajili kwa kuwapora Yanga, Try Again alisema wana uwezo mkubwa wa kuweza kusajili mchezaji yeyote wanayemtaka ndani ya timu hiyo.
“Nashangazwa na kauli za kudai waliporwa kiungo wa timu hiyo Fabrice Ngoma jambo ambalo halina ukweli wowote, Simba inapotaka mchezaji yeyote haiwezi kumkosa. Hizi stori za kuwa tumemchukuwa uwanja wa ndege ni maneno tu, maana tulimaliza dili la Ngoma wiki moja kabla ya kutua hapa nchini, kumpata haikuwa ngumu kwa sababu ya uhusiano mzuri kati yetu na Al Hilal,” alisema na kuongeza:
“Ngoma ni mchezaji bora kwa Afrika, tumeweza kumnunua licha ya kukutana na vita vikubwa kutoka klabu zingine na si yeye hata usajili wa Willy Essomba Onana ulikuwa na changamoto kubwa siku ambayo tumemsajili kuna klabu ya Kaskazini mwa Afrika ikamtumia ujumbe kwenye simu yake ya mkononi na kumsumbua meneja wake kuachana na ofa yetu na kupewa pesa mara tatu zaidi tutakayompa, ulikuwa ugomvi mkubwa ingawa tuliweza kumbakisha.”










