Mashindano hayo yatawashirikisha vijana waliokuwa wanatumia dawa za kulevya na kupata nafuu kupitia vituo vya tiba ya Methadone na 'Soba House' kutoka Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano cha Taasisi ya Kurunzi ya Jamii, Aziz Suleiman alisema mashindano hayo yanatarajiwa kuanza mwezi Mei mwaka huu na kuhitimishwa Siku ya Kimataifa ya kukabiliana na Dawa za Kulevya Duniani Juni 26,2023.
Alisema Kurunzi ya Jamii inaunga mkono juhudi za serikali, wadau wa maendeleo na mashirika ya kimataifa katika kuzuia matumizi ya dawa za kulevya nchini.
"Katika mashindano haya timu itakayoshinda,itazawadiwa mradi wa kimaendeleo utakaowapatia kipato cha kujikimu kiuchumi ambacho kitarudisha heshima yao kwa jami na familia zao, kwa tathmini fupi tulioifanya baadhi ya wanufaika wa tiba ya Methadone na Soba House hurudia matumizi ya dawa za kulevya kwa sababu ya ukosefu wa ajira na jamii kutokubaliana nao kama watu waliopata nafuu," alisema.
Aliongeza kuwa katika kipindi ambacho mashindano ya "Zinduka Cup" yanaendelea kutakua na hamasa mbalimbali ambazo zitakua zinatolewa kwa jamii kupitia vyombo mbalimbali vya habari haswa mitandao ya kijamii.
Alisema kuwa hamasa hizo zitatolewa na watu mashuhuri nchini wakiwemo wasanii wa Bongo Flava wa zamani na wasasa ilikuvutia mashindano hayo na kutoa elimu ya madhara ya matumizi ya dawa za kulevya kwa jamii.
Aliwataja baadhi ya wasanii hao kuwa ni Inspector Haroon "Babu" na msanii wa singeli Barobaro
Alisema kuwa mashindano hayo yatakua yakifanyika kila mwaka na yatakua yakihitimishwa siku ya kukabiliana na matumizi ya dawa za kulevya duniani.
Kurunzi ya Jamii inafungua fursa kwa kampuni za kibiashara, vituo vya televisheni, taasisi za serikali na zisizo za kiserikali kuunganisha nguvu ya pamoja ili kufanikisha mashindano haya, na kuwa nufaisha vijana wanaopata nafuu ya uraibu wa dawa za kulevya na kurudi kulitumikia taifa, familia zao na hata kurudisha imani yao kwa jamii.










