Maarufu FA Cup pamoja na kumaliza nafasi tatu za juu Ligi Kuu Bara ili kuwa miongoni mwa zitakazopata nafasi hiyo.
Timu tatu zitakazomaliza nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, zitakata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa inayoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.
Hata hivyo, timu itakayomaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu, inaweza kupata nafasi ya kushiriki michuano hiyo ya CAF, endapo tu timu itakayotwaa Kombe la FA, itakuwa ndiyo iliyobeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara, jambo ambalo limeongeza ushindani mkubwa kwenye ligi hiyo kila moja ikiwania nafasi hiyo ya kushiriki michuano ya kimataifa.
Bingwa wa Ligi Kuu na mshindi wa wa pili huiwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa wakati mshindi wa Kombe la FA na itakayoshika nafasi ya tatu, hupeperusha bendera ya nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Singida Big Stars, John Kadutu, alisema mikakati yao ni kuhakikisha wanashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na kutwaa Kombe la Shirikisho, FA Cup.
"Malengo yetu ni kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam," alisema Kadutu.
Mtendaji huyo aliweka wazi kuwa kila mchezo kwao ni fainali na kuahidi kupata pointi tatu kwenye michezo iliyobakia kabla ya ligi hiyo kufikia ukingoni.
Alisema kutokana na juhudi zinazoonyeshwa na wachezaji wao wana matumaini ya kushiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika hapo mwakani.
"Tutapambana kuhakikisha mwakani tunashiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, hakuna linaloshindikana," alisema mtendaji huyo.










