Rais Samia kuipa Stars mil. 500/- ikifuzu Afcon

21Mar 2023
Saada Akida
DAR ES SALAAM
Nipashe
Rais Samia kuipa Stars mil. 500/- ikifuzu Afcon

BAADA ya hamasa aliyoitoa kwa Klabu za Simba na Yanga kwenye michuano ya kimataifa kuendelea kuzaa matunda ya ushindi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan

Sasa ameigeukia Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars na kuiahidi mamilioni endapo itafuzu Fainali za Mataifa ya Afrika, Afcon 2023.

Rais Samia aliahidi na ameendelea kutekeleza kutoa Sh. milioni tano kwa kila goli litakalofungwa na Simba na Yanga kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika ambapo hadi sasa timu hizo zimeshalamba jumla ya Sh. milioni 85.

Simba inayopeperusha bendera ya Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, imeshalamba milioni 45 huku Yanga yenye dhamana hiyo kwa upande wa Kombe la Shirikisho, ikiondoka na milioni 40.

Kupitia kwa Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Pindi Chana, Rais Samia ametoa ahadi ya Sh. milioni 500 kwa Taifa Stars, endapo ikifuzu kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika, Afcon 2023 ziakazofanyika nchini Ivory Coast.

Taifa Stars tayari imeshawasilini nchini Misri kujiandaa na mchezo dhidi ya Timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes) utakaopigwa Ijumaa wiki hii katika Uwanja wa Ismailia, kabla ya timu hizo kurudiana Machi 28, mwaka huu katika Dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana katika Ukumbi wa Benjamin Mkapa, Waziri Dk. Pindi, alisema Rais Samia anaendelea kutoa hamasa na ameahidi kutoa Sh. milioni 500 endapo Stars itafanikiwa kufuzu fainali hizo.

Alisema huo ni mwendelezo wa hamasa ambazo anazitoa kwa timu zinazofanya vizuri katika michuano ya kimataifa na sasa ameahidi fungu hilo kwa Taifa Stars.

“Tayari serikali imefanikiwa kumleta Kocha mpya, Adel Amrouche, yuko nchini Misri na timu inayojiandaa na mchezo wetu dhidi ya Uganda kuhakikisha tunapata ushindi katika mechi hiyo kabla ya kurudiana Machi 28, mwaka huu hapa nyumbani,” alisema na aliongeza:

"Wachezaji wanatakiwa kupambana kuhakikisha tunafanikiwa kurejea na ushindi katika mchezo huo na ninamwagiza Naibu Waziri wangu, Hamis Mwinjuma (Mwana FA), kuongoza msafara na kwenda nchini humo kuongeza nguvu katika safu ya viongozi na wadau watakaokwenda nchini Misri,” alisema Dk. Pindi.

Katika mechi hizo za kuwania kufuzu Afcon, Taifa Stars ipo Kundi F sambamba na Algeria, Niger na Uganda, ambapo timu mbili zitakazomaliza nafasi ya juu zitafuzu moja kwa moja kushiriki fainali hizo.

Algeria ndiyo inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi sita, ikifuatiwa na Niger yenye alama mbili huku Tanzania na Uganda zikifuata kutokana na kulingana kila kitu zikiwa na alama moja kila moja