Idd Azzan aunga mkono vita rushwa ya ngono

29Nov 2023
Sabato Kasika
DAR ES SALAAM
Nipashe
Idd Azzan aunga mkono vita rushwa ya ngono

MADAU michezo, Idd Azzan ameunga mkono vita ya rushwa ya ngono inayoendeshwa na shirika la Wanawake Katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI) na kuyataka makundi ya jogging kuunga mkono vita hiyo.

Idd Azzan akihutubia makundi ya jogging. PICHA SABATO KASIKA.

Azzan ameunga mkono juhudi wakati akipokea makundi mbalimbali ya jogging ya mkoa wa Dar es Salaam kwenye uwanja wa michezo wa Shule ya Msingi Tandale, baada kumaliza mbio za kilomita tano.

Katika hotuba yake kwa makundi hayo, amesema michezo ni afya, na kwamba vijana kuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vya ukatili huo ndani ya makundi hayo na katika jamii.

"Vitendo vya rushwa ya ngono vimekuwa vikitajwa kufanyika ndani ya jamii, na kwamba makundi ya jogging yasiruhusu vitendo hivyo kujitokeza katika makundi yenu," amesema Azzan.

Mkurugenzi wa WAJIKI, Janeth Mawinza, amesema wanashirikiana na makundi ya jogging ya mkoa wa Dar es Salaam, katika vita dhidi ya rushwa ya ngono kupitia kampeni ya 'Safari Salama Bila Rushwa ya Ngono Inawezekana', waliofadhiliwa na Women Fund Tanzania (WFT).

"Tulianza kuwashirikisha makundi ya jogging machache na sasa yameongezeka baada ya kuona umuhimu wa vita ya rushwa ya ngono, ninaamini tunakwenda vizuri kupeleka elimu hii," amesema Janeth.

Katibu wa umoja wa vilabu 10 vya jogging Kinondoni, Vincent Kikube amesema makundi hayo yanaunga mkono wito wa Azan wa kupinga rushwa ya ngono kwa kuwa unajua madhara yake.

"Ni kweli kuna tatizo hilo katika jamii, nasi tulishaanza kutoa elimu ya kupambana nayo baada ya kufundisha na watalaamu kutoka shirika la WAJIKI," amesema Kikube.

Mwanachama wa Barafu Jogging ya Magomeni Haruna Magumbo, amesema yeye kama mzazi na pia mwanamichezo, anakerwa na ukatili huo,¹ huku akiahidi kuhamasisha vita hiyo katika kundi lake.