Shabiki ampiga refa, timu yapokwa pointi na faini juu

29Nov 2023
Hawa Abdallah
Zanzibar
Nipashe
Shabiki ampiga refa, timu yapokwa pointi na faini juu

KAMATI ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi ya Bodi ya Ligi Zanzibar, imetoa alama tatu na mabao mawili kwa Zimamoto SC baada ya shabiki wa timu ya Kundemba FC kumpiga mwamuzi pembeni (mshika kibendera namba mbili) na kusababisha mchezo huo kuvunjika ndani ya dakika za nyongeza.

Katika mchezo huo ulichezwa Novemba 22, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mau hadi unavunjika timu hizo zilikuwa zimetoshana nguvu kwa kufungana mabao 2-2.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kamati hiyo na kutiwa saini na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Zanzibar, Issa Kassim, imeeleza kuwa maamuzi hayo yaliyotolewa ni kwa mujibu wa Kanuni ya Mashindano ya ZFF sura ya 20 (6) na sura ya 27 (1) (2) (3), (i), (ii) na (4).

Taarifa hiyo ilieleza kuwa mbali na adhabu hiyo, timu ya Kundemba FC imepigwa faini ya Sh. milioni tano ambapo Sh. milioni moja ni kwa sababu ya kufanya fujo zilizosababisha kuvunjika mchezo huo na Sh. milioni nne, ametozwa shabiki wake aliyemshambulia mwamuzi wa mchezo huo.

Aidha, wachezaji wa timu ya Kundemba FC, Ally Makame, amefungiwa mechi tatu, huku Issa Ramadhani akifungiwa mechi moja kwa kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu katika mchezo huo.

Hata hivyo, kamati hiyo ambayo ipo chini ya Bodi ya Ligi Zanzibar,  imeipa siku saba timu ya Kundemba  FC kuhakikisha inalipa faini hizo.