-akichezea klabu tano tofauti.
Straika huyo amesajiliwa siku moja tu baada ya Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha kulalamika kuwa kwa sasa anakosa mshambuliaji mwenye uwezo wa kupachika mabao na mwenye nguvu ya kukabiliana na mabeki wababe ndani ya eneo la hatari.
Rekodi zinaonesha kuwa Jobe alifunga mabao 23 na ‘asisti’ tano, katika mechi 28 kwenye Ligi Kuu ya Bangladesh. Katika Ligi Kuu ya Kazakhstan akifunga mabao 13 na ‘asisti’ tano katika michezo 25 aliyocheza.
Jobe akiwa katika Ligi Kuu ya Macedonia Kaskazini alifunga mabao matatu katika mechi 12 wakati kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kabla ya kutua timu hiyo ya Ulaya alifunga mabao mawili katika mechi nne huku Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa hajaziona nyavu katika michezo miwilii aliyocheza.
Katika maisha yake ya soka, klabu alizozichezea Jobe ni pamoja na Shkendija na Struga za nchini Macedonia, msimu wa 2022/23 alijiunga na Klabu ya Neman Grodno ya nchini Beralus kabla ya kujiunga na Zhenis na sasa Simba.
Kabla ya hapo, Mgambia huyo alianza kuzichezea Klabu za Tallinding United FC ya nchini mwao, 2011 hadi 2014, alipotimkia kwenye Klabu ya ASEC Ndiambour ya Senegal, 2017 hadi 2019 ambapo alicheza michuano ya Afrika Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.
Akizungumza wakati akitambulishwa Simba, Jobe hakuwa na maneno mengi zaidi ya kusema “nipo hapa kwa ajili ya kufunga mabao”.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu hiyo, Salim Abdallah 'Try Again', amesema wameongeza mchezaji mwingine wa nafasi hiyo kwa ajili ya kuongeza nguvu na kuwasukuma waliopo ili waweze kufanya vizuri.
"Tumeongeza mchezaji mwingine wa nafasi ya ushambuliaji kuja kuongeza nguvu katika eneo hilo tunamkaribisha sana Jobe," alisema Try Again.
Kusajiliwa kwa straika huyo kutafanya safu ya ushambuliaji ya Simba kuwa na mastraika wanne, na kumpa wigo mpaka kocha, ambapo kwa sasa ina nahodha John Bocco, Jean Baleke na Moses Phiri.
Hata hivyo, kwa siku za karibuni, mastraika hao wote wameonekana kutokuwa kwenye kiwango chao cha kawaida kiasi cha kumfanya Benchikha kulalamika kupatiwa straika mwingine haraka.
Wakati huo huo, Klabu ya Simba imesema kocha wao Benchikha ameonekana kufurahishwa na michuano ya Kombe la Mapinduzi kwani imempa nafasi ya kujua mchezaji gani wa kubaki na wa kuondoka yeye mwenyewe bila kuambiwa na mtu.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally amesema licha ya kutopata ubingwa, lakini kocha wao Benchikha ameonekana kuyafurahia mashindano hayo kwani ameshuhudia mwenyewe kwa macho yake viwango vya wachezaji wake wote, hivyo atafanya maamuzi yeye mwenyewe.
"Benchika amesema amepata muda mrefu wa kuwaona wachezaji wake na hasa wale ambao wamekuwa hawapati namba kwenye kikosi cha kwanza, ametuambia amemwona Luis Miqussone akirejea kwenye kiwango na pia amepata muda wa kumtazama Hussein Kazi akisema ni hazina, lakini amesema kuna wachezaji ambao hajaridhika nao na atawaacha.
"Hii yote ni kwa sababu ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, vinginevyo sijui ingekuwaje, kwa hiyo kaeni mkao wa kujua tukaoachana nao, tayari mwalimu amewapa nafasi baadhi ya wachezaji na amejiridhisha kuwa hawawezi kumsaidia kwenye safari yake huko mbele," alisema Ahmed.










