Xavi awaomba radhi mashabiki Barcelona

17Jan 2024
RIYADH, Saudi Arabia
Nipashe
Xavi awaomba radhi mashabiki Barcelona
  • Ni kushindwa kugumu, Madrid walifanya uharibifu mkubwa kwenye...

KOCHA wa Barcelona, Xavi Hernandez, ameomba msamaha kwa mashabiki wa klabu hiyo baada ya kuchapwa mabao 4-1 na Real Madrid Jumapili kwenye fainali ya Kombe la Supercopa nchini Saudi Arabia.

KOCHA wa Barcelona, Xavi Hernandez.

Vinicius Junior alifunga hat-trick kipindi cha kwanza katika Uwanja wa Al-Awwal Park, mabao mawili ndani ya dakika 10 za kwanza, naye Rodrygo Goes akakamilisha kipigo hicho kipindi cha pili huku Madrid wakilipiza kisasi kwa Barca kwa kushindwa mwaka jana kwenye fainali hiyo.

Robert Lewandowski alikuwa ameisaidia Barca kwa muda kurejea mchezoni wakati wakiwa nyuma kwa mabao 2-1, lakini bao la tatu la Vinicius, kupitia mkwaju wa penalti, liliondoa matumain kabla ya mapumziko.

"Nimesikitishwa na nina huzuni," alisema akiiambia Movistar baada ya mechi.

"Hili ni soka na leo tunapaswa kukabiliana na upande mchungu wa mchezo.

"Ni aibu, tulikuwa na matumaini makubwa kwenda fainali na tumetoa matokeo mabaya zaidi. Tulianza vibaya, tulipata nafasi ya kurejea, lakini penalti iliua mchezo.

"Hatukuwa na raha. Madrid walifanya uharibifu mkubwa kwenye kaunta na katika kipindi cha mpito. Tunaomba radhi kwa mashabiki, hatukushindana, lakini nimepata vipigo vingi na klabu hii."

Xavi aliomba msamaha kutoka kwa mashabiki mara kadhaa katika mkutano wake na waandishi wa habari baada ya mchezo na akasema yuko tayari kwa ukosoaji ambao "utastahili" kufuata.

"Ni wakati wa kusema pole kwa mashabiki na kukubali ukosoaji unaokuja," aliongeza. "Hatukuonesha upande wa timu ambayo tunapaswa kuwa nayo kwenye fainali, haswa dhidi ya Madrid.

"Tulikuwa katika hali mbaya zaidi na ni kombe lililopotea. Ninawajibika. Ninakubali kukosolewa na tutaendelea kufanya kazi kwa bidii.

"Ni kushindwa kugumu, lakini tumepona kutoka kwa kushindwa mara nyingi hapo awali na tutashindana tena kwa njia bora zaidi."

Hata hivyo, licha ya hali ya matokeo hayo, pamoja na kuwa nyuma kwa pointi nane kwa vinara wa LaLiga, Girona, Xavi, ambaye aliiongoza Barca kutwaa ubingwa wa ligi mwaka jana, hahofii kibarua chake.

"(Kuna kujiamini, ndio," alisema bosi wa Barca, ambaye aliongeza mkataba wake hadi 2025 mwaka jana, alisema alipoulizwa kama bado anaungwa mkono na uongozi wa klabu.

"Lazima tujikosoe na kusahihisha mengi, lakini bado naamini katika mradi huo na unaweza kuwa na msimu mzuri. Tunapaswa kujikosoa sana juu ya utendaji wetu leo.

"Kuna sababu za kuamini, tulishinda mataji mawili mwaka jana nikiwa kocha, si zamani, ilikuwa ngumu naomba radhi kwa mashabiki, lakini kuna mabishano ya upande wetu.”