Kikosi cha Yanga kinaendelea na maandalizi ya mchezo huo watakaokuwa ugenini Ijumaa wiki hii katika Uwanja wa Julai 5, 1962 (Stade du 5 Juillet 1962) nchini humo kuhakikisha wanaanza vizuri hatua ya makundi.
Akizungumza na Nipashe, Gamondi alisema ana matarajio ya kuingia katika mchezo huo kwa mbinu nyingine tofauti ikiwamo kufanya mabadiliko ya kikosi kwa sababu anatambua CR Belouizdad nao wamekuwa wakiwafuatilia tangu makundi yalipopangwa.
Alisema licha ya wao kuwafuatilia CR Belouizdad katika michezo yao, pia Yanga wamekuwa wakifuatiliwa kwa umakini, hivyo atahakikisha anafanya mabadiliko ya kikosi katika mchezo huo wa ugenini.
“Mabadiliko ya kikosi yatakuwapo, wachezaji watakapokamilika wote kila mmoja atakuwa anajua majukumu yake, katika mchezo huo hatutaingia kama ilivyo kwa michezo mingine tuliocheza awali,” alisema Gamondi.
Aliongeza kuwa yuko makini katika kuimarisha kikosi chake katika kila sekta zaidi washambuliaji ambao tayari amefanyia kazi na sasa yupo na safu ya ulinzi kulingana na uimara wa washambuliaji wa CR Belouizdad.
“Nimewafuatilia baadhi ya michezo yao wakicheza, nao wamefanikiwa kufunga bao kila mechi, hilo tuko nalo makini kuhakikisha haturuhusu bao. Kufikia huko lazima tujiweke sawa kila eneo na kuwakumbusha mabeki kuwa makini.
"Kikosi kipo vizuri licha ya wachezaji wengine kuwapo kwenye majukumu ya timu zao za taifa, waliobaki wanafanyia kazi majukumu yao ili kujiweka imara zaidi ya mechi zilizopita,” alisema kocha huyo.
Alisisitiza kuwa wamejiandaa kwa mapambano ya aina yote kwa kila mchezaji kufanya kazi kwa ushirikiana mkubwa ili kufikia malengo wanayoyatarajia kwa msimu huu.
Kocha huyo alisema anachohitaji ni kupata ushindi katika mchezo wa kwanza, na kwamba anaamini akianza vizuri haitokuwa kazi kubwa kwenye michezo inayofuata.
Wachezaji wa timu hiyo walipata mapumziko ya siku moja na leo wanarejea kwenye uwanja wa mazoezi kuendelea na maandalizi ya mechi hiyo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.









