ya kirafiki dhidi ya Dar City kwenye Uwanja wa Mo Arena, wakishinda 4-0.
Cadena, ambaye baada ya kuichukua Simba iliyokuwa chini ya Roberto Oliveira aliyeondoshwa kutokana na kipigo cha mabao 5-1 Novemba 5, mwaka huu, alibainisha wazi kuwa katika jambo linalomkera ni timu hiyo kuruhusu bao na mabao karibuni kwenye kila mechi inayocheza iwe ya Ligi ya Mabingwa, African Football League, Ligi Kuu Tanzania Bara na hata mechi za kirafiki.
Baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Namungo kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, kocha huyo aliainisha ni kitu gani ataanza nacho kwenye mazoezi na kinaonekana kimeanza kufanyiwa kazi.
"Kwa sasa kazi yangu kubwa kuelekea kwenye mchezo ujao ni kuisuka beki, nataka kupunguza baadhi ya makosa na mapungufu ya kuruhusu mabao, kwa timu kubwa kama yetu si vema kuwa na tabia hiyo kwa sababu mara kwa mara tunacheza na timu kubwa ambazo hutumia makosa madogo ambayo yanafanyika kukuadhibu," alisema.
Jana asubuhi, Cadena alionekana kusisitiza kukaba kwa ushirikiano, huku mabeki wakitakiwa kutofanya makosa ya kujirudia.
Kwenye mechi hiyo ya kirafiki, kocha aliwachezesha baadhi ya wachezaji ambao wamekuwa hawapati nafasi kama Abdallah Khamis, David Kameta na Nassor Kapama.
Wadau wa soka wakiongozwa na rais wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage, waliokuwa wakipendekeza Che Fondoh Malone achezeshwe kama kiungo mkabaji, hawakukosea kwani alianza kuifungia timu hiyo bao la kwanza dakika ya 40, akipata pasi kutoka kwa Mohamed Hussein 'Tshabalala.'
Willy Onana, ambaye inasemekana huenda akaonyeshwa mlango wa kutokea kipindi cha dirisha dogo kwa kushindwa kuwashawishi mabosi wake na hata mashabiki, alifunga bao la pili kwa mkwaju wa penalti, Israel Patrick akifunga bao la tatu kabla ya Moses Phiri kuhitimisha idadi ya mabao kwa kufunga la nne dakika ya 75 baada ya kupokea pasi ya kisigino kutoka kwa nahodha John Bocco.
Simba inaelekea kwenye mechi hiyo ya hatua ya makundi bila kocha mkuu, ambapo ndoto za kumpata kabla ya mechi hiyo kama ilivyokuwa inadaiwa na viongozi wa klabu hiyo zinaelekea kufifia.










