Kwa mujibu wa takwimu za Dawati la Michezo la Nipashe ni mabao manane ya vichwa yamefungwa mpaka sasa, ambapo kati ya hayo Azam imefunga mawili kupitia wachezaji wake Idd Selemani 'Nado' na Feisal Salum.
Feisal alifunga bao la kichwa Agosti 16, Azam ilipoisulubu Tabora United mabao 4-0, wakati Nado alifanya hivyo Septemba 21, mwaka huu, akipachika bao la pili la ushindi, Azam ikiifunga Singida Fountain Gate 2-1, Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Timu nyingine zenye mabao yaliyofungwa kwa kichwa ni Simba, bao lake likiwekwa wavuni na Fabrice Ngoma kwenye mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu, Uwanja wa Manungu Complex, Turiani mkoani Morogoro, Simba ikipata ushindi wa mabao 4-2 Agosti 15, mwaka huu.
Zingine ni JKT Tanzania kupitia Edward Songo, KMC wakifungiwa na Juma Shemvuni, Namungo kwa bao la Pius Buswita, Geita Gold kwa bao la Elius Maguri, na Ihefu ambayo bao lake la kichwa lilifungwa na Lenny Kisu kwenye mechi ambayo ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Yanga.
Timu ambazo mpaka sasa hazijaonja ladha ya mabao ya vichwa ni Yanga, Mashujaa, Singida Fountain Gate, Coastal Union, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Tabora United, Prisons na Dodoma Jiji.
Wakati huo huo takwimu zikionyesha mpaka sasa penalti sita zimetoka, tano zikiwekwa wavuni, ambapo Bodi ya Ligi imetoa majina ya wachezaji sita waliosababisha penalti hizo.
Wachezaji hao ni Moses Phiri na Luis Miquissone wa Simba, Shiza Ramadhani 'Kichuya' wa Namungo, Antony Mlingo wa Geita Gold, Edson Katanga wa JKT Tanzania na Impiri Mbombo wa Tabora United.
Kwa mujibu wa takwimu zetu, penalti hizo ziliwekwa wavuni na Fabrice Ngoye wa Namungo, Jean Baleke na Saidi Ntibazonkiza wa Simba, Daniel Lyanga wa JKT Tanzania na Erick Okutu wa Tabora United, huku Elius Maguri wa Geita Gold akikosa penalti yake.









