Yanga kuitumia mechi ya Simba kuimaliza Al Ahly

19Oct 2023
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga kuitumia mechi ya Simba kuimaliza Al Ahly
  • Gamondi na benchi zima kuhamia kwa Mkapa Ijumaa na 'diary' zao...

WAKATI Simba ikitarajia kucheza mechi ya ufunguzi ya michuano ya African Football League (AFL) keshokutwa, Ijumaa dhidi ya Al Ahly ya Misri, benchi la ufundi la Yanga nalo linajipanga kwa ajili ya kuhakikisha linautazama kwa makini mchezo huo kwa ajili ya kupata mbinu za kucheza na timu hiyo-

-katika mchezo wao wa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Taarifa zilizopatikana ndani ya kambi ya timu hiyo, zimeeleza kuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi na timu yake ya wataalam wa kuchambua na kusoma mbinu za michezo ya wapinzani, watakuwa uwanjani siku hiyo kwa kazi moja tu ya kuratibu kila kitu kinachoendelea, ikiwamo mfumo watakaoutumia na hata kujua wachezaji hatari wa kuchungwa.

Habari zimeeleza kuwa benchi la ufundi la Yanga limeamua kuutumia mchezo huo kwa sababu mechi wakatayocheza Desemba Mosi, mwaka huu itakuwa hapa nchini, hivyo wana uhakika kuwa watapata uwezo sahihi wa Al Ahly wanapocheza ugenini ikiwamo kuhimili hali ya hewa ya Dar es Salaam.

"Kila kitu watakachofanya hapa kwenye mechi dhidi ya Simba kitakuwa sahihi kwetu kujifunza kwa sababu hawatobadilika wakija tena kucheza hapa, mfumo watakaotumia, spidi yao, na hata uhimili wa hali ya hewa ya hapa," kilisema chanzo hicho.

Yanga ipo Kundi D pamoja na Al Ahly, CR Belouzdad ya Algeria na Medeama ya Ghana.

"Ni kweli Simba inacheza dhidi ya Al Ahly kwenye michuamo ya AFL, lakini pambano hili linaweza kuwa na manufaa makubwa kwa Yanga, kwa sababu baada ya hapo tayari tutakuwa tumeshajua uimara na udhaifu wa Al Ahly hii mpya, hasa ikicheza ugenini kwenye maeneo ya joto kama haya," alisema mtoa habari huyo.

Naye Makamu wa Rais wa klabu hiyo, Arafat Haji, ametamba kuwa kwa sasa wana kikosi kizuri ambacho kinaweza kushindana na timu kubwa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwamo Al Ahly.

"Al Ahly ni timu nzuri na itakuwa inatetea ubingwa, lakini sisi tunatakiwa kuonesha kwamba tunastahili kushindana nao na kushinda mechi ya nyumbani na ugenini, tuna kikosi kizuri cha kupambana nao," alisema Arafat.

Alisema kama uongozi siku zote wameendelea kulipa benchi la ufundi uhuru na mahitaji muhimu na wameendelea kuliamini.

Timu yetu ipo tayari kwa Ligi ya Mabingwa, tuna wachezaji katika Timu ya Taifa ya Tanzania na wapo wachezaji wengine wenye uzoefu wa kutosha, hivyo tunaamini pia tunaweza kufanya vizuri kwenye michezo yetu ya Kundi D tulilopangwa,” alisema.

Simba ni timu pekee katoka Ukanada wa Afrika Mashariki (CECAFA), ambayo inashiriki michuano hiyo AFL inayoshirikisha timu nane bora zaidi barani Afrika huku mechi yao dhidi ya Al Ahly ikiwa ni ufunguzi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Timu zingine zinazoshiriki michuano hiyo AFL ni pamoja na Wydad Casablanca (Morocco), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Esperance Tunis (Tunisia), Petro Atletico de Luanda (Angola), Enyimba FC (Nigeria) na TP Mazembe (DR Congo).