Timu hiyo ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) ina nafasi kubwa ya kukutana na Wanalambalamba hao baada ya kushinda mabao 3-0 dhidi ya Light Stars ya Shelisheli katika mechi yao ya kwanza ya raundi ya awali ya michuano hiyo.
Bidvest itakuwa mwenyeji katika mechi ya marudiano jijini Johannesburg, Afrika Kusini wikiendi hii.
Mchezo wa kwanza kati ya Azam FC na Bidvest Wits utachezwa Machi 12 mwaka huu kwenye Uwanja wa Bidvest jijini Johannesburg saa 12.00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki kabla ya kurudiana nao Azam Complex Machi 20 mwaka huu saa 9.00 alasiri.
Katika kuhakikisha wanafanya vizuri, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema jana kuwa watapiga kambi maalumu kwenye nchi jirani na Afrika Kusini kwa siku nne kabla ya kwenda jijini Johannesburg siku moja kabla ya mchezo huo.
Kiongozi huyo alisema kuwa mara baada ya mchezo huo, watarajea kambini kwenye nchini walioichagua kuendelea na maandalizi na watatua jijini Dar es Salaam siku moja kabla ya mechi yao ya kiporo ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Stand United itakayochezwa Azam Complex Machi 16.
Kuruhusiwa kwa Azam FC kupiga kambi nje ya nchi kutavuruga kwa mara nyingine ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na timu hiyo ya Chamazi kuwa na mechi ya ligi ugenini mkoani Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar Machi 9.










