Chad, Stars sasa kuvaana Machi 23

25Feb 2016
Somoe Ng'itu
Dar
Nipashe
Chad, Stars sasa kuvaana Machi 23

MECHI ya kwanza ya kuwania kufuzu kushiriki fainali zijazo la Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) kati ya Chad na wageni Taifa Stars itachezwa Machi 23 badala ya Machi 25 kama ilivyopangwa awali, imefahamika.

Kocha mkuu wa Taifa Stars, Boniface Mkwasa.

Timu hizo zilizoko Kundi G pamoja na Misri na Nigeria, zitarudiana Machi 28 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kocha mkuu wa Taifa Stars, Boniface Mkwasa, aliiambia Nipashe jana kuwa wamepokea taarifa za mabadiliko ya siku hiyo ya mchezo na sasa kikosi chake kitasafiri kuelekea N'Djamena Machi 21.

Mkwasa alisema anaomba Mungu wachezaji anaowahitaji wasipate majeraha yoyote kwa sababu hatakuwa na muda wa kuita nyota wapya kwa kuwa hakuna muda wa kufanya mazoezi ya pamoja.

"Itabidi niite wachezaji ambao wameiva na walioko tayari kwa kupambana, hatutakuwa na muda hata wa kufanya mazoezi ya pamoja, tutakutana Machi 20 jioni na siku inayofuata tutakuwa safarini," alisema Mkwasa.

Aliongeza kuwa nyota wengi anaotarajia kuwajumuisha kikosini, wanatoka kwenye klabu za Yanga na Azam ambao watakuwa wametoka kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.