Azam FC yaenda Tunisia kwa mafungu

16Apr 2016
Faustine Feliciane
Dar
Nipashe
Azam FC yaenda Tunisia kwa mafungu

KUNDI la kwanza la wachezaji na viongozi wa timu ya Azam FC limesafiri jana kuelekea Tunisia kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa mashindano ya Kombe la Shirikisho utakayofanyika Jumanne Aprili 19 mjini Tunis.

Afisa Mtendaji wa timu hiyo, Saad Kawemba alisema jijini Dar es Salaam kuwa uamuzi wa kusafiri kwa 'mafungu' unalenga kukwepa 'hujuma' dhidi ya Waarabu hao ambao mara kadhaa wamekuwa na vitendo vya 'figisufigisu' dhidi ya timu pinzani.

"Kikubwa ni kukwepa hujuma za wapinzani wetu hakuna sababu nyingine, tumeona tusingeweza kusafirisha 'mara yote katika kapu moja'," alisema Kawemba.

Kiongozi huyo alisema kundi la kwanza la timu hiyo liliondoka nchini jana likiwa na idadi ya watu 17 ambao baadhi yake viongozi na wachezaji wa timu hiyo huku kundi lingine likitarajiwa kusafiri leo na kesho.

Kikosi hicho cha Kocha Stewart Hall kinahitaji sare au ushindi wa aina yoyote ili waweze kusonga mbele kufuatia ushindi wa magoli 2-1 walioupata kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika Aprili 10 kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini.