Arsenal ndiyo mabingwa watetezi wa michuano hiyo baada ya kufanikiwa kutetea ubingwa wao msimu uliopita walipoichapa Aston Villa mabao 4-0 katika mechi ya fainali. Na kwa mara ya tatu mfululizo wanakutana, Hull ina matumaini ya kuwatupa nje ya michuano hiyo.
Gunners walitoka nyuma kwa mabao 2-0 na kushinda 3-2 dhidi yao katika fainali ya 2014 kwenye Uwanja wa Wembley na kisha wakashinda 2-0 mwaka jana katika raundi ya tatu.
Huku wakikabiliwa na mechi ngumu dhidi ya Barca wiki ijayo, haitashangaza kuona Wenger anapumzisha nyota wake wengi wa kikosi cha kwanza wakati Hull watakapotua kwenye Uwanja wa Emirates wikendi hii ili kujipanga vyema kwa ajili ya mechi ya Jumanne. (AFP)










