Patachimbika leo

20Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Patachimbika leo
  • Simba imeshinda mechi zote saba za Ligi Kuu ilizocheza mwaka 2016 wakati Yanga hawajapoteza mechi hata moja kwenye Uwanja wa Taifa msimu huu.

LIGI Kuu Tanzania Bara inaendelea leo kwa mechi tano, lakini macho na masikio ya wengi yataelekezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar e Salaam katika mechi ya pili ya watani wa jadi msimu huu.

MASHABIKI WA YANGA

Simba ambayo imeshinda mechi zote nane (saba za Ligi Kuu) ilizocheza chini ya kocha mkuu wa muda, Jackson Mayanja, itakuwa na kibarua kigumu kulipa kulipa kisasi cha kufungwa mabao 2-0 duru la kwanza dhidi ya Yanga ambao hawajapoteza mechi hata moja kwenye Uwanja wa Taifa msimu huu.

Baada ya kushinda mechi mbili zilizopita za Ligi Kuu mkoani Shinyanga dhidi ya Kagera Sugar na Stand United, kikosi cha Wanamsimbazi kilipiga kambi kwenye Chuo cha Biblia eneo la Bigwa mkoani Morogoro kujipanga kuwakabili Yanga ambao walipitiliza Pemba baada ya kurejea nchini Jumapili wakitokea Mauritius walikocheza mechi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Cercle de Joachim.

Simba walirejea Dar es Salaam juzi juzi usiku wakati Yanga waliwasili mchana wa siku hiyo na timu zote zimefikia kwenye hoteli za nyota tano katikati ya jiji.

Kocha Mholanzi wa Yanga, Hans van der Pluijm amekwepa kutanguliza majigambo kuelekea mchezo, wakati mpinzani wake (Mayanja) hajasita kutamba atashinda hata 3-0.

Mganda huyo anasema baada ya kuiona Yanga katika mechi kadhaa za hivi karibuni zikiwamo ilizochapwa na Coastal Union kabla kulazimishwa sare ya 2-2 na Tanzania Prisons, amegundua ni timu anayoweza kuifunga kwa urahisi.

Pluijm amewapa heshima yao Simba kwamba ni timu ambayo imeimarika kwa sasa na anaamini mchezo utakuwa mgumu hii leo na hasa akizingatia atawakosa mabeki wake wazoefu wa kati, Kelvin Yondani anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu na nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye bado ni majeruhi.

Mara ya mwisho timu zilipokutana katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, Yanga ilishinda 2-0 Septemba 26, mabao ya Amissi Tambwe na Malimi Busungu.

Mayanja ameiongoza Simba kushinda mechi zote sita za Ligi Kuu tangu arithi mikoba ya Muingereza Dylan Kerr Januari 10, wakati Pluijm ambaye yupo Yanga tangu mwaka 2014 amepoteza mchezo mmoja tu msimu huu akifungwa 2-0 na Coastal Union Januari 30, mwaka huu.

Takwimu za Nipashe zinaonyesha kuwa ukikiondoka kipigo cha 2-0 dhidi ya Yanga na sare ya 2-2 dhidi ya Azam FC, Simba imeshinda mechi zingine zote nane ilizochezwa kwenye Uwanja wa Taifa msimu huu ikifunga magoli 25 na kufungwa sita.

Pia ukiitoa sare ya 1-1 dhidi ya Azam FC, takwimu zinaibeba Yanga kufanya kweli dhidi ya Simba Jumamosi kutokana na kushinda mechi zingine zote 10 ilizochezwa kwenye Uwanja wa Taifa msimu huu wakitupia magoli 33 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara tatu.

Vikosi vinatarajiwa kuwa; Yanga; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Mwinyi Mngwali, Donald Ngoma, Haruna Niyonzima na Deus Kaseke.

Simba; Vincent Angban, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Juuko Murshid, Justice Majavbi, Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Ibrahim Hajib, Hamisi Kiiza na Awadh Juma.