‘Date my Family’ kuonekana rasmi

02Jul 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
‘Date my Family’ kuonekana rasmi

KATIKA kufundisha kuelekea katika maisha mapya, kipindi cha mahusiano kijulikanacho kwa jina la ‘Date my family’ kitaanza kuonyeshwa kwenye Chaneli ya Maisha Magic Bongo iliyoko DSTV kuanzia leo na kitaonekana katika vifurushi vyote, imefahamika.

Mwandaaji wa filamu nchini, Aziz Mohamed akiwa na baadhi ya wasanii na wadau wa sanaa wakati wa uzinduzi wa kipindi kipya cha mahusiano cha ‘Date my Family’ ambacho kitaanza kuonyeshwa kuanzia leo kwenye king'amuzi cha chaneli ya Miasha Magic Bongo ya DSTV. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Kipindi hiki cha aina yake cha mahusiano humuonyesha kijana katika hatua zake za kuchumbia lakini tofauti na ilivyozoeleka, hapa kijana atakuwa anawasiliana na familia za wachumba watarajiwa na hatimaye kufanya uamuzi wa mchumba kabla hata hawajaonana.

 “Date My Familiy ni kipindi kinachohusu mahusiano hivyo kinawaunganisha watu  wenye tabia zinazofanana, ambapo kijana anayetaka mchumba atakutana na familia tatu tofauti zenye wachumba watarajiwa na baada ya mazungumzo na familia hizo mchumbiaji ataamua kumposa mchumba mmoja,” alisema Ronald Shelukindo, Mkuu wa Masoko wa MultiChoice Tanzania.

Kulingana na mazungumzo ya kina baina ya mchumbiaji mwenyewe na familia ya mchumba, kijana atapata fursa ya kumfahamu vizuri mchumba wake bila kumuona.

“Baada ya kukutana na familia hizo, mabachela au warembo hao watachagua familia waipendayo na hatimaye kwenda kukutana na mchumba husika,” alisema Shelukindo.

Aliongeza kipindi hicho kitakuwa na burudani ya aina yake ambayo yenye kuonyesha visa na mikasa kuanzia hatua ya kuongea na familia hadi hatua ya mwisho ya kukutanishwa na mchumba. 

“Kama ulivyo msisitizo wetu sisi Maisha Magic Bongo, asilimia kubwa ya maudhui yetu ni ya Kitanzania na huzalishwa hapa na wazalishaji Watanzania. Tunaamini kwa uzoefu wao watazalisha tena kipindi bora na kitakuwa burudani kubwa kwa watazamaji ndani na nje ya nchi,” alisisitiza Shelukindo.