Waluguru Original wana Morogoro Yetu

17Jun 2020
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Waluguru Original wana Morogoro Yetu

BENDI ya muziki wa dansi ya Waluguru Original yenye maskani yake mjini Morogoro, imekamilisha nyimbo sita, ikiwa ni maandalizi ya albamu mpya kwa mwaka huu wa 2020.

Deogtratius Killer (mwenye shati nyeupe), akicheza na wanenguaji wake kwenye onyesho la bendi hiyo mwishoni mwa wiki mjini Morogoro. PICHA: SABATO KASIKA

Mkurugenzi wa bendi hiyo, Deogratius David 'Killer' alizitaja nyimbo hizo kuwa ni 'Morogoro Yetu, Mwanzo wa Mapenzi, Cha Kupewa, Ngalile Mwanangu Ndole, Supu na Nataka Nilewe.'

Killer alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na gazeti hili na kufafanua kuwa Waliguru Original iliandaa nyimbo hizo kabla ya shughuli za burudanu kusimamishwa ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.

"Baada ya maambukizi ya corona kupungua, tumeanza maonyesho na pia tunajiandaa kwa ajili ya kurekodi nyimbo zetu ikiwa ni maandalizi ya albamu mpya kwa mwaka huu wa 2020," alisema Killer.

Mwanamuziki huyo alisema, mbali na hayo wanaendelea kuimarisha bendi yao ambayo amedai kuwa imekuwa tishio kwa bendi nyingine za muziki wa dansi mjini Morogoro na maeneo mengine ya Tanzania.

Alisema, sasa ni wakati wao wa kuendelea kujiimarisha zaidi kwa ajili ya kuwapa burudani safi mashabiki wao ambao waliikosa kwa muda mrefu mara maonyesho yaliposimamishwa.