Baada ya mchezo huu, wiki ijayo, Agosti 17, mwaka huu timu zote 16 zinazoshiriki ligi hiyo zitaanza mbio za kuwania taji hilo linaloshikiliwa na Yanga ya jijini Dar es Salaam.
Yanga ilitwaa ubingwa huo kwa kuwavua watani zao, Simba ambao walikuwa wanaushikilia kwa msimu wa nne mfululizo.
Mshindi wa taji hilo na timu inayoshika nafasi ya pili, zinapata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na kusimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Msimu uliopita, Yanga inayofundishwa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi, raia wa Tunisia ilitwaa ubingwa huo kwa kuweka rekodi ya kutofungwa, lakini ikijihakikishia ubingwa ikiwa imebakiza mechi tatu mkononi.
Hata hivyo, kazi kwa Yanga haikuwa nyepesi, ilikutana na changamoto mbalimbali katika mbio hizo za kutimiza malengo yake.
Yanga ilipambana katika kila mechi, iliweka msimamo kwamba kila mchezo kwake ni fainali na kauli mbiu hiyo ilichangia kuongeza morari kwa wachezaji, viongozi, wanachama na mashabiki.
Hata hivyo, Yanga haikufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ya CAF kwa kutolewa kwenye hatua za mapema wakati wapinzani wao, Simba wakiishia hatua ya robo fainali.
Baada ya maandalizi yao ya msimu mpya, sasa timu hizo zinakutana kwa mara ya kwanza msimu huu kwenye mchezo huu wa Ngao ya Jamii.
Kwa maandalizi yaliyofanywa na timu zote mbili ikiwemo mechi zao za kimataifa katika matamasha yao ya Siku ya Wananchi na Simba Day, Nipashe tunaamini kwamba, mchezo wa leo utakuwa wa kiwango cha juu na uliojaa ujuzi pamoja na ubora wa kimataifa.
Tunasema hivyo kwa sababu, timu zote mbili baada ya mechi zao za kujifua na zile za hivi karibuni za kimataifa dhidi ya Vipers ya Uganda na St. George ya Ethiopia, zimeona na kufanyia kazi mapungufu yaliyoonekana na benchi la ufundi.
Yanga kwenye kilele chao cha siku ya Wananchi ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-0, wakati watani zao Simba waliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Nipashe tunaamini kwamba, mabenchi ya ufundi ya Yanga na Simba yameona madhaifu ya timu zao na kila mmoja amejipanga vizuri zaidi kuelekea kuchezo huu wa leo utakaopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa.
Nipashe hatutarajii kuona mchezo huo ukikosa ladha na burudani kwa wachezaji kucheza kwa shinikizo au mhemuko kutokana na ukubwa wa mchezo wenyewe, kwani huu ndio wakati wa kuonesha ubora wa vikosi vyao.
Na pia ni wakati wa wachezaji wapya kuonesha uwezo wao na kujiwekea imani kwa makocha wao kuwa na uhakika wa kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
Zote Yanga na Simba zimefanya usajili mkubwa kwa kuimarisha na kuboresha vikosi vyao, hivyo leo sio siku ya majaribio bali ni siku ya kufanya kweli kwa wachezaji kuonesha ujuzi wao uwanjani.
Tunaamini kitakachooneshwa leo kwenye mchezo huu, ndio kitakuwa ufunguzi wa mechi nyingine nzuri zaidi katika mzunguko wa Ligi Kuu hadi kufikia mwisho wake.
Nipashe inazitakia Yanga na Simba mechi yenye kiwango, ufundi na ubora na tunaamini wachezaji pamoja na benchi la ufundi watalizingatia hilo ili mashabiki waweze kupata burudani nzuri na kuufurahia mchezo wenyewe.









