Agizo hilo la Rais lilitokana na kushuhudia kinamama wengi wafanyabiashara, wakifanya shughuli zao huku wakiwa wamebeba watoto wao mgongoni.
Rais Samia, alisema kitendo hicho sio tu kinawaathiri watoto, bali hata wazazi wao ambao baadaye wanaweza kupata madhara katika miili yao.
Akizungumza katika ufunguzi huo, Rais Samia alisema ameona kinamama wengi wamebeba watoto migongoni na kushauri itakuwa vizuri wakamegewa sehemu ya soko hilo wakaweka eneo la kuangalia watoto ili wakati mama yupo kazini na biashara zake watoto hao wawe wanashughulikiwa mahala pazuri, wanapata chakula vizuri, wanakua vizuri, wanapata elimu huku wanatunzwa vizuri.
Alimwagiza Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya kuangalia nafasi nzuri kwa ajili ya watoto hao.
Agizo hilo la Rais limekuja wakati mwafaka kutokana na kinamama wengi wafanyabiashara iwe ya sokoni, mamalishe au kutembeza bidhaa barabarani, kutembea na watoto wao kwenye shughuli zao, pengine wanafanya hivyo kwa kukosa msaada wa kulea watoto hao nyumbani.
Athari za watoto kuambatana na wazazi sehemu za biashara ni watoto kuiga tabia ambazo haziendani na umri wao.
Tumeshuhudia sehemu zenye mikusanyiko ya watu hasa sokoni, kuna watu wenye tabia tofauti kwa kutoa lugha na vitendo vizisivyofaa bila kujali kuna watoto.
Pia, watoto wanapata mateso ya kukosa haki yao ya kucheza na kupata elimu kutokana na muda mwingi kuambatana na mama zao kwenye shughuli zao za biashara.
Watoto hao pia wanakuwa katika mazingira hatarishi kwa sababu maeneo ambayo wanawekwa wakati wazazi wao wakiendelea na shughuli sio rafiki kwao.
Agizo la Rais la kutaka maeneo ya soko kutengwa vyumba maalumu vya kutunzia watoto hao, litasaidia kupata haki yao ya kufurahia uhuru wao kucheza na watoto wenzao, kupata matunzo mazuri na pia kupata chakula kizuri, kama alivyopendekeza Rais.
Mtoto anapozoea mazingira yasiyoendana na umri wake, kwa vyoyote anabeba tabia anazoziona kila siku na kukua nazo, na inapotokea kuwa ni mbaya matokeo yake ni kuwa mtoto mwenye tabia mbaya.
Unaweza kukuta mtoto anatoa matamshi au vitendo ambavyo haviendani na umri wake kwasababu tu amezoea kusikia wakubwa wakitamka na kwake kuona ni sawa.
Ni vizuri maeneo ambayo wajasiriamli kinamama wanaokosa msaada wa malezi kwa watoto wao majumbani mwao, wakajengewa vituo vitakavyowasaidia watoto wao kuondokana na athari zitakazoathiri maisha yao ya baadaye.
Ni matumaini yetu kuwa agizo lililotolewa na Rais Samia, litakuwa chachu kwa maeneo yote ambayo wafanyabiashara kinamama, watatengewa eneo la kuweka watoto wao na mwalimu atayewasaidia kuwapa elimu na kukua katika malezi mema na mazingira mazuri.