Tamasha hilo, pamoja na mambo mengine, lilikuwa na lengo la kutambulisha kikosi chake kipya kwa ajili ya msimu wa Ligi Kuu ya NBC mwaka 2022/23 pamoja na michuano ya kimataifa.
Kama ilivyo ada, tamasha hilo hutanguliwa na burudani mbalimbali kama vile muziki kutoka kwa wasanii mbalimbali na ubunifu kutoka kwa mashabiki.
Sambamba na mambo hayo, tamasha hilo huhitimishwa na mechi kati ya Simba na timu iliyoalikwa mahususi kwa ajili ya kunogesha tamasha hilo na kuwapa burudani wapenzi na kuonyesha umahiri wa kikosi kipya kilichosajiliwa. Kwa mwaka huu, Simba iliialika timu ya St. George kutoka Ethiopia na kuiadhibu kwa mabao 2-0.
Pamoja na mambo hayo, tamasha hilo liliibua taharuki baada ya msanii Tunda Man kuingia uwanjani akiwa amebebwa kwenye jeneza, kukiwa na msalaba na mtu aliyeigiza kama kiongozi wa dini ya Kikristo, aliyevaa joho na stola huku mkononi akiwa amebeba Biblia. Baada ya kufika uwanjani, aliyevaa mavazi ya kichungaji, alibainisha kwamba ndani ya sanduku hilo kuna mtu ambaye alifariki dunia Agosti 6, mwaka huu, na chanzo cha kifo chake ni maneno aliyokuwa akiyatoa.
Tarehe hiyo ambayo pia ilionyeshwa kwenye msalaba, ilikuwa siku ambayo Yanga ilikuwa na kilele cha Wiki ya Wananchi na ilicheza mechi kati yake na Vipers ya Uganda na kufungwa mabao 2-0. Kutokana na matokeo hayo, watu hao waliingia na jeneza uwanjani, walikuwa kama wanaigiza utani kama ilivyo jadi kwa klabu hizo mbili kongwe nchini hasa baada ya Yanga kufungwa.
Licha ya kuwa ulionekana ni utani, suala hilo limeibua taharuki kwa watu mbalimbali wakiwamo baadhi ya viongozi wa dini ambao wameweka bayana kwamba suala hilo ni kejeli, dharau na unajisi dhidi ya dini ya Kikristo kwa kile kilichoelezwa kuwa kwa imani ya dini hiyo, msalaba ni ishara ya ukombozi kwa waumini wao.
Baadhi ya viongozi wa dini walikwenda mbali zaidi kwa kusema watu wanaoigiza mambo kama hayo na kufanya dhihaka mbele ya Mwenyezi Mungu, hawana mwisho mwema na kitendo hicho kinaashiria maafa katika jamii ikiwamo misiba na majanga ya asili.
Kutokana na kitendo hicho, serikali tayari imeshachukua hatua kadhaa ikiwamo kumwondoa katika nafasi yake meneja wa uwanja kwa kile kilichoelezwa kushindwa kutekeleza masuala la kiusalama katika eneo hilo.
Kwa ujumla, kitendo hicho si tu kwamba ni cha fedheha na dhihaka dhidi ya Ukristo bali kwa watu wa imani zote kwa kuwa kimeshusha na kudhalilisha heshima ya dini na hata waumini wake.
Ni vyema serikali ikachukua hatua madhubuti kudhibiti vitendo kama hivyo kwa kuwa licha ya kudhalilisha na kukashfu imani mojawapo, kinaweza kusababisha machafuko katika jamii ikiwamo kuzuka mvutano baina ya dini moja na nyingine na kusababisha maafa. Tunapaswa kujifunza katika mataifa mengine ambayo migogoro ya kidini imesababisha kuwapo kwa umwagaji wa damu dhidi ya watu wasio na hatia.
Vitendo kama hivyo vya kuigiza vimekuwa vikifanywa katika mechi baina ya Yanga na Simba pamoja na wasanii wa tamthilia mbalimbali nchini. Ufike wakati sasa serikali ipige marufuku vitendo hivyo kwa kuwa havina mwisho mwema.









