Hongera TPLB kuruhusu 12 wote kucheza Ligi Kuu

15Aug 2022
Mhariri
Nipashe
 Hongera TPLB kuruhusu 12 wote kucheza Ligi Kuu

SASA imefika wakati mchezaji mwenye uwezo, mwenye nidhamu na anayejituma ndiye atakayecheza mechi. Hii ni baada ya Bodi ya Ligi nchini (TPLB), kuruhusu kutumika kwa wachezaji wote 12 wa kigeni kwa mechi moja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari ya Mawasiliano ya Bodi ya Ligi, imesema, hilo limepitishwa na Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), katika kikao ilichoketi Agosti 9, mwaka huu jijini Arusha, ambapo kimepitia maboresho ya kanuni za Ligi Kuu, ambayo wadau wengi walipendekeza kipengele hicho.

Kabla ya maboresho hayo, klabu zilikuwa zinaruhusiwa kusajili wachezaji wa kigeni wasiozidi 12, lakini ziliruhusiwa kutumia wachezaji wanane katika mchezo mmoja.

Hiki kilikuwa ni kilio cha muda mrefu kwa wadau wa soka ambao walikuwa wanahoji ni kwa nini klabu ziruhusiwe kusajili wachezaji 12, lakini ni wanane tu waruhusiwe kwa mechi moja.

Yaani klabu inasajili wachezaji, inawalipia vibali vya kufanya kazi na pia vya kuishi nchini, lakini kwenye kila mechi ni lazima wanne wakae jukwaani, ni kanuni ambayo ilikuwa haitendi haki na ikizipotezea klabu pesa nyingi bila sababu yoyote. Kama ingeendelea ingekuwa haina maana, badala yake ni bora klabu zingeruhusiwa kusajili wachezaji wageni ambao idadi yake inaruhusiwa kuwatumia.

Ina maana klabu zingepunguziwa wachezaji kutoka 12 hadi nane, au kuacha wote watumike. Kabla ya kanuni hiyo kupitishwa, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almasi Kasongo, alibainisha kuwa wanakwenda kupitisha kanuni ambazo ni rafiki kwa wadau na ambazo wengi wamezipendekeza.

Nitoe pongezi kwa TFF, TPLB na kamati yake kwa kusikiliza maoni ya wadau wengi wa soka ambao walikuwa wakiliangalia hili kwa jicho la tatu. Baadhi waliona kwamba litawanyima fursa wachezaji wa kizawa ambao watakosa namba kwenye vikosi mbalimbali kwenye klabu zao.

Hawa ndiyo wanataka wachezaji wa Kitanzania wawe na upendeleo maalum hata kama hawana uwezo mzuri na wageni wabanwe, licha ya kwamba wana uwezo.

Kwa hili lililopitishwa, kwa maoni yangu, siyo kwamba litawaumiza wachezaji wa Kitanzania, la hasha. Kilichofanyika ni kwamba kila mchezaji, awe wa Kitanzania au mgeni acheze kulingana na uwezo wake na si kanuni imbebe.

Hapa ni kwamba Mtanzania anatakiwa ajitume ili apate namba na si kusubiri wageni wapunguzwe na kanuni ili yeye acheze.

Sidhani kama kuna kocha yeyote atakuwa akiwaweka tu uwanjani wachezaji 11 wa kigeni na mmoja nje kwa sababu wanatoka nje ya nchi, hapana. Makocha watakuwa wanapanga timu kutokana na uwezo wa kila mchezaji, hivyo kilichobaki ni wote kupigania namba.

Hii pia ni kengele ya hatari inaanza kugonga kwa wachezaji wazawa, ambao baadhi yao wamebaki kucheza kwa mazoea, kwani makocha watakuwa wakichagua wachezaji wenye uwezo na wenye kujituma mazoezini tu bila kujali anatoka wapi.

Nasema ni kengele ya hatari kwenye vichwa vya wachezaji wa ndani, kwani kanuni hiyo imepitishwa wakati ambapo si Simba, Yanga wala Azam pekee ambazo zimesajili wachezaji wengi wa kigeni, bali hata zile timu ambazo hakuna yeyote aliyeamini kuwa watashusha 'maproo' kama Polisi Tanzania, Prisons, Mtibwa Sugar, Coastal Union, achilia mbali Namungo, Ihefu na Singida Big Stars.

Hii inaonyesha kuwa hakuna masihara, wachezaji wa Kitanzania wanatakiwa sasa kuvuta soksi ili kuwanyang'anya namba wageni kwa uwezo wao uwanjani.

Kwa hiyo wanatakiwa kujituma mazoezini, kuwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja na kupunguza anasa ambazo huwafanya leo wacheze vizuri, lakini kesho wakionekana si kama siyo yule wa jana.