Juzi wakala huo ulitoa taarifa kuwa uko tayari kudhamini watu hao kupitia mikopo itakayotolewa na benki ili kuwawezesha kuanzisha vituo hivyo.
Katika taarifa hiyo ilielezwa kuwa, zaidi ya Shilingi bilioni mbili zitakopeshwa kwa wananchi wanaotaka kuanzisha vituo hivyo maeneo ya vijijini, ili kuhakikisha usalama wa watu na bidhaa yenyewe kwa vyombo vya usafiri na mitambo.
Wakala huo umesema, kwa sasa wanakamilisha taratibu za kutoa mikopo hiyo na kuwatambua waombaji, maeneo yatakayowekwa vituo na kuhakikisha tathmini ya uharibifu wa mazingira imefanyika.
Tangu kuanzishwa kwa REA mwaka 2007 zaidi ya Shilingi trilioni tatu zimetumika kusambaza nishati hiyo vijijini, pia kuchangia ukuaji wa uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na maendeleo vijijini kwa asilimia 25.
Mkurugenzi Mkuu wa REA, Hassan Saidi na Mkurugenzi wa Uendeshaji Masoko na Teknolojia, Advera Mwijage, wakati wakizungumzia majukumu, changamoto na mafanikio ya wakala tangu kuanzishwa kwake, walihakikisha wananchi kuwa wamefikia uamuzi huo kutokana na mwenendo wa uuzaji mafuta vijijini ambao ni holela na hatarishi kwa maisha ya watu na kuharibu vyombo vya usafiri na kwamba utaratibu utakaotumika ni kuwaunganisha na benki ziwakopeshe.
Uuzaji wa nishati hiyo katika maeneo mbalimbali hasa ya vijijini ni kuweka kwenye magaloni ndani ya nyumba ambako ni hatari kama yatakuwa karibu na moto na kulipuka.
Katika baadhi ya maeneo pia, uuzaji huo hutumika kwa kuwekwa kwenye chupa za maji zilizotumika na kupangwa barabarani huku zikipigwa na jua, hali ambayo pia ina hatarisha usalama wa watu na pia kupunguza thamani ya bidhaa yenyewe.
Viongozi hao waliwataka wananchi wauze mafuta kwa utaratibu mzuri na usafi na lengo la kuja na mpango huo wa mikopo ni kuwadhamini kwa mwaka huu wa fedha.
Fursa hii ilitolewa na REA haina budi kuchangamkiwa kwasababu pamoja na kuepusha madhara katika makazi ya watu pia inatoa ajira kwa vijana.
Sio wafanyabiashara wote wanaouza mafuta kwa njia holela wanapenda kufanya hivyo, wengine wanashindwa kufungua vituo rasmi kwasababu ya kukosa uwezo wa kufungua vituo hivyo.
Mpango huo wa REA wa kuwadhamini wananchi utatoa fursa kwa wale waliokuwa na mitaji midogo kujiongezea na kufungua vituo rasmi vya kuuzia nishati hiyo.
Vijiji vingi nchini vinakosa huduma ya vituo rasmi vya kuuzia mafuta na huduma pekee wanayopata ni kwa njia ya kuuziwa kwenye chupa.
Ukiangalia vijana wengi wamejiajiri katika kazi ya udereva wa bodaboda na bajaji na hutegemea nishati hiyo kutoa huduma kwa wateja.
Wakisogezewa huduma salama kwenye maeneo yao itawakomboa wengi na pia kuwaepushia vyombo vyao kupata madhara kutokana na kuwa na njia isiyo salama ya kuuziwa mafuta.
Ni matumaini yetu kuwa wananchi watachangamkia fursa hiyo ambayo pia itasaidia kuongeza ajira kwa vijana.









