Chonde chonde madereva epukeni vilevi

17Aug 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Chonde chonde madereva epukeni vilevi

SIKU za hivi karibuni kumetokea mfululizo wa matukio ya ajali za barabarani kwa kupoteza maisha ya watu wengi na wengine kuachwa na majeraha au ulemavu wa kudumu.

Matukio hayo ya ajali baadhi yanasababishwa na mwendo kasi na uzembe wa madereva kutozingatia alama za barabarani.

Pia baadhi ya madereva kugundulika kwenye magari yao kuwa na vilevi hali inayoonesha kuwa wanaendesha huku wakitumia vilevi hivyo.

Utumiaji wa vilevi ukiwa unaendesha gari lazima utaleta madhara kwa sababu dereva anashindwa kudhibiti ajali inapotokea kutokana na kutokuwa na umakini.

Kilevi kinapotumika hata kwa mtu anayetembea kwa miguu kinaonekana kumyumbisha na kukosa mwelekeo wa kule anakoelekea na gari hivyo huwa mbaya zaidi kwasababu ya kasi ya chombo kushindwa kukidhibiti.

Pamoja na madereva kukemewa kuhusu tabia hiyo, lakini baadhi wanaonekana kupuuza na kuendelea kupoteza maisha ya watu wasiokuwa na hatia.

Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa, limeamua kuwaonya madereva wa vyombo vya moto kujihusisha na matumizi ya pombe wawapo barabarani.

Akitoa onyo hilo, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Noah Mwakyoma, alisema mkoa wa Iringa umejipanga kukabiliana na ajali za barabarani kwa kuwadhibiti madereva wenye tabia hiyo.

Akitaja sababu mbalimbali zinazochagiza kuongezeka kwa ajali za barabarani anasema ni pamoja na matumizi ya pombe na dawa za kulevya kwa madereva wakati wakiwa wanaendesha vyombo vya moto.

Anasema wako baadhi ya madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani na wakati mwingine makosa yao husababisha ajali na kukatisha uhai wa watu na wengine kupata ulemavu wa kudumu kitu ambacho hakikubaliki.

Mkakati uliowekwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa ni  kuwachukulia hatua za kisheria madereva wote watakaobainika kukiuka sheria za usalama barabarani ili iwe funzo kwa wengine wenye tabia hiyo.

Kadhalika, jeshi hilo linaendelea kuwapima madereva kabla ya kuanza safari ili kupunguza ajali za barabarani zitokanazo na ulevi na kuwachukulia hatua wale wanaobainika.

Madereva wanaotajwa zaidi kutumia vilezi wakati wanapokuwa kwenye vyombo vya moto ni wanaoendesha bodaboda na bajaji.

Vile vile, madereva hao wanakiuka viwango vya kubeba abiria wanavyotakiwa kwenye vyombo hivyo kwa kuongeza idadi.

Kwa mfano pikipiki inatakiwa kubeba abiria mmoja, lakini baadhi ya madereva hupakiza abiria wanne pamoja na dereva idadi inakuwa watu watano sawa na gari ndogo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni, takriban watu 1,191 walifariki dunia na 2,139 kujeruhiwa kutokana na ajali za barabarani 1,594 zilizotokea nchini kati ya Julai mwaka 2021 na Machi mwaka 2022.

Idadi hii ya vifo ni kubwa na ukiangalia baadhi yao wameacha familia ambazo zilikuwa zikiwategemea.

Baadhi ya watu wamepoteza familia nzima na kuachwa wapweke na wengine kuwa na ulemavu wa kudumu.

Ni jukumu la madereva, abiria kuwa makini wanapokuwa barabarani. Abiria wana haki ya kumwonya dereva anapoonekana kufanya vitendo vitakavyosababisha ajali.

Elimu pia inatakiwa kutolewa mara kwa mara na ufuatiliaji kwa madereva ili kudhibiti ajali. Wananchi ni wajibu wao kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwasababu wao ndiyo waathirika wakubwa zinapotokea ajali.