Licha ya kusababisha madhara hayo, ajali hizo pia zimekuwa chanzo cha kupotea kwa nguvu kazi ya taifa, uharibifu wa magari na hasara katika kampuni za bima.
Juzi, mathalani, watu 19 walifariki dunia na wengine kujeruhiwa baada ya lori lililokuwa limesheheni mchanga wa dhahabu likitokea Chunya mkoani Mbeya kwenda Dar es Salaam, kufeli breki katika mteremko wa Inyala jijini Mbeya na kuparamia magari matatu.
Magari hayo yaliyogongwa na lori hilo, ni pamoja na basi moja la abiria linalofanya safari kati ya Mbeya na Njombe na idadi kubwa ya waliopoteza maisha walikuwa katika basi hilo.
Licha ya sababu zinazoelezwa kila ajali inapotokea kuwa baadhi ya magari kufeli breki, vyanzo vingine vimekuwa vikitajwa kuwa ni mwendokasi wa madereva, matumizi ya vilevi na ubovu wa magari.
Katika ajali ya juzi, taarifa mpya zilizotolewa na polisi jana zilibainisha kuwa lori lililosababisha maafa hayo lilikuwa bovu na hilo lilibainika baada ya polisi kikosi cha usalama barabarani kufanya ukaguzi. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, dereva wa lori hilo ambaye alikimbia baada ya kusababisha ajali, anadaiwa kukimbia na sasa anasakwa ili achukuliwe hatua za kisheria.
Kutokana na sababu hiyo, kunaibuka maswali mengi ambayo baadhi yanakosa majibu. Moja ya maswali hayo ni, je, ilikuwaje polisi wakaruhusu gari hilo kuendelea na safari ilhali limebainika kuwa ni bovu? Swali la pili, ni kwa nini dereva akaidi mbele ya polisi wakati chombo hicho kina mamlaka ya kuchukua hatua za kulisimamisha kuendelea na safari hadi kasoro zilizojitokeza zitakaporekebishwa?
Ukakasi uliomo katika maswali hayo, unatokana na ukweli kwamba Jeshi la Polisi hususan Kikosi cha Usalama Barabarani, limekuwa likitajwa mara kwa mara kuwa ni moja ya taasisi ambazo zimekithiri katika tuhuma za rushwa. Kwa msingi huo inawezekana kuna mazingira ya rushwa yalikuwapo hadi gari hilo kuendelea na safari ilhali lilibainika kuwa ni bovu.
Kwa msingi huo, kuna mazingira yanayojionyesha kuwa polisi kwa namna yoyote ile wanahusika katika ajali hiyo. Tunasema hivyo kwa sababu taarifa waliyoitoa imebainisha kuwa dereva alikaidi! Dereva anakaidi vipi mbele ya chombo cha dola na akaachwa bila kuchukuliwa hatua?
Kwa mazingira hayo, ni wakati mwafaka sasa kwa Jeshi la Polisi hususan kikosi chake cha usalama barabarani kujitathmini na kurejea katika mstari wake na kutekeleza majukumu yake ili kulinda maisha ya watu ambayo kwa sasa yako hatarini kutokana na ajali ambazo zimetamalaki na zinatokea kila uchao. Licha ya kutekeleza majukumu ipasavyo, pia askari walioruhusu gari hilo kuendelea na safari pamoja na kuwa bovu, wachukuliwe hatua.
Ni imani kwamba iwapo Jeshi la Polisi litasimamia kanuni, taratibu na sheria zinazosimamia usalama barabarani, ajali ambazo zimekithiri sasa zitapungua kwa kiasi kikubwa. Ni vyema polisi wakatekeleza wajibu wao kama ulivyoainishwa kwa mujibu wa sheria, kwa maana ya usalama wa raia na mali zao.









