Utalii ni neema, lakini huduma ziboreshwe

19Aug 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Utalii ni neema, lakini huduma ziboreshwe

HABARI njema ya kufurika kwa watalii nchini ichukuliwe kama changamoto kwa sekta inayosimamia jukumu hilo kuboresha huduma zake.

Haitapendeza watalii wanapoingia nchini na kukuta huduma zisizoridhisha, itawavunja moyo wa kurudi tena na hata kuwatangazia wenzao waliotamani kuja kuona vivutio vinavyotangazwa kupitia filamu ya Royal Tour, ambayo Rais Samia Suluhu Hassan ameitangaza ulimwenguni na Tanzania kutambulika kwa vivutio vyake.

Tunaposema huduma tunamaanisha kuanzia ukarimu wa kukaribisha wageni kwa kutumia lugha rafiki itakayowafanya wajisikie wako nyumbani. Suala la huduma kwa wateja kwa baadhi ya watoa huduma linalalamikiwa sana.

Ndiyo maana kuna umuhimu wa kwenda kwenye vyuo vinavyofundisha masuala ya utoaji huduma kuanzia kwenye ofisi, hotelini, sehemu za mapokezi wakati wageni wanapoingia na kutoka nchini.

Mapokezi ni sehemu muhimu itakayomfanya mgeni atambue kama huduma aliyoifuata ataipata kama alivyoitarajia.

Ni vizuri pia hoteli zinazopokea wageni zikiwa kwenye usafi wa hali ya juu. Kuna baadhi ya hoteli mgeni anapoingia chumbani anaanza kukerwa na harufu ya uvundo au kukutana na wadudu kama mende, vyoo visivyoridhisha na wakati mwingine kukosekana kwa huduma ya maji na umeme.

Hata Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, ambaye alitembelea Hifadhi ya Mikumi kuzindua malori 44 na mitambo 18 ya shughuli za utalii Kusini mwa Tanzania kupitia mradi wa REGROW, aliwataka wafanyakazi wa hoteli za kitalii kuwa wakarimu wazuri kwa wageni ili wapeleke sifa nzuri ya nchi.

Tanzania ni kati ya nchi zinazokabiliwa na tatizo la ukosefu wa ajira, fursa hii ya utalii inaweza kuwa mkombozi mkubwa wa ajira zilizo rasmi na zisizo rasmi.

Kupitia utalii, watu wanaweza kupata fursa ya kuuza bidhaa zao wanazozitengeneza ambazo licha ya kuwapatia kipato, lakini zinakwenda kutangaza nchi yao, watalii wanapokwenda nazo kwao.

Ajira zipo za aina mbalimbali kwenye hoteli za kitalii kuanzia kwenye usafi, uhudumu hadi kazi za ofisini kwa wageni na nyingine nyingi.

Hata hivyo, wakati mwingine fursa hizo Watanzania wanazikosa kwasababu ya vitu vidogo vidogo vya kutowajali wateja na wakati mwingine lugha huwa tatizo la mawasiliano.

 Ndiyo maana baadhi ya wawekezaji huamua kuchukua watu wao na kuwapa ajira, huku Watanzania wakibaki kulalamika.

Mfano mzuri ni wenzetu wa nchi jirani ambao kwenye sekta ya huduma kwa wateja wanafanya vizuri na baadhi ya wawekezaji kuamua kuwachukua kwa sababu wana lugha pia ya kushawishi wateja.

Mteja anapokwenda kupata huduma fulani akaikosa, angependa kupewa njia nyingine ya kupata huduma hiyo badala ya kumuacha na kumpoteza.

Huduma za usafiri pia ni muhimu kwa wageni wanaokuja kutembelea nchi yetu, watoa huduma hiyo pia wanatakiwa kuwa wakarimu kwa wageni na wasitumie fursa kwa kufanya udanganyifu wa kuwatoza fedha nyinyi wanapotaka kwenda sehemu moja kwenda nyingine.

Nchi yetu imebarikiwa kuwa nchi ya amani na watu wenye upendo, hivyo tutumie tunu hizi kuwafanya wageni wetu watamani kuja kutembelea Tanzania kila wakati.